Castro azikwa, Cuba yaingia kipindi baada ya Fidel
4 Desemba 2016Baada ya wiki za kutoa rambirambi na maandamano ya umma, majivu ya Castro yatazikwa katika eneo la makaburi la Santa Ifigenia mjini Santiago de Cuba, mji ulioko mashariki mwa nchi hiyo , ambako hatua za mapinduzi zilianzishwa zaidi ya nusu karne iliyopita.
Rais Raul Castro aliongoza mkutano mkubwa wa mwisho kwa heshima ya kaka yake katika eneo la uwanja wa mapinduzi wa Santiago Plaza jana Jumamosi, akiongoza umati wa watu kwa kuahidi kuendeleza mapinduzi.
"Mbele ya mabaki ya mwili wa Fidel .. tunaapa kulinda ardhi ya baba zetu na ujamaa," Raul Castro alisema. "Ameonesha kwamba , ndio tutaweza, ndio tunaweza, ndio tutavuka vikwazo vyovyote, kitisho, misukosuko katika nia yetu thabiti kujenga ujamaa nchini Cuba," alisema.
Alama za kuabudiwa
Castro aliyefariki Novemba 25 akiwa na umri wa miaka 90 atazikwa , katika tukio "dogo la kawaida" karibu na kaburi la shujaa wa uhuru wa karne ya 19 Jose Marti, Castro alisema.
Lakini bunge la taifa , ambalo linakutana baadaye mwezi huu, litaidhinisha sheria kutimiza ombi la Castro wakati akifariki kwamba hakutawekwa sanamu kwa ajili ya kumbukumbu yake ama mtaa ambao utaitwa kwa jina lake , alisema.
"Kiongozi wa mapinduzi amekataa kila aina ya kumtukuza," Raul Castro alisema.
Wakati Castro alikaa kanda kwa muda mrefu kutokana na upasuaji katika utumbo muongo mmoja uliopita, ameendelea kuwa mtu muhimu nchini Cuba.
Aliheshimiwa na waungaji wake mkono kutokana na kutoa matibabu bure pamoja na elimu bure aliyoisambaza katika kisiwa hicho, na alichukiwa na wapinzani ambao walimuona kama dikteza katili.
Huzuni na masikitiko
Mazishi yake yanakamilisha kipindi cha siku nne za maombolezi ambamo Wacuba , mara kadhaa wakihamasishwa na serikali, walimiminika mitaani kutoa heshima zao kwa Castro, wakiimba "mimi ni Fidel" wakati majivu ya mwili wake yakichukuliwa kupita katika nchi hiyo kuelekea katika mazishi.
"Nina masikitiko makubwa kwasababu tumempoteza baba," alisema marta Loida , profesa wa chuo kikuu mwenye umri wa miaka 35 akiwa amekaa chini akishikilia picha ya Fidel Castro baada ya hotuba ya Raul.
"Ni kama hatutaki kusema kwaheri," amesema . "Tunataka kuendelea kuwa nae usiku kucha chini ya nyota."
Serikali ililea hamasa hii ambayo imekuwa kama ya kidini, huku vyombo vya habari vya serikali vikimuita Castro "kamanda wa milele."
Katika wiki moja iliyopita , Wacuba walihimizwa kwenda shuleni na maeneo mengine ya majengo ya umma kutia saini kiapo cha kuwa watiifu kwa mapinduzi yake.
"Namuamini Raul kwasababu Raul ni kaka yake Fidel. Fidel alimfundisha kila kitu," alisema Irina Hierro Rodriguez, mwalimu mwenye umri wa miaka 23 katika mkutano wa Jumamosi.
Licha ya kuwa Raul Castro alitoa ahadi kama hiyo, ametekeleza mageuzi kiasi ya kiuchumi katika miaka ya hivi karibuni, akirejesha uhusiano wa kidiplomasia na Marekani na kuapa kwamba atajiuzulu mwaka 2018.
"Akiwa hayuko tena chini ya kivuli cha kaka yake , Raul huenda sasa akajihisi kuwa huru zaidi kuendelea na mageuzi ya kiuchumi aliyoyaanzisha muongo mmoja uliopita," alisema Jorge Duany, mkurugenzi wa taasisi ya utafiti ya Cuba katika chuo kikuu cha kimatifa cha Florida nchini Marekani.
Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe
Mhariri: Isaac Gamba