Watakaomtukana rais watachukuliwa hatua Tanzania
23 Julai 2019Kauli hiyo kali imetolewa na Katibu Mkuu wa CCM taifa Dr Bashiru Ally mjini Dodoma wakati akihutubia katika shughuli ya uzinduzi wa miradi ya CCM.
Dr Bashiru amesema kumezuka tabia ya ajabu kwa baadhi ya wanachama wa chama hicho kutoa maneno ya matusi na kejeli kwa Raisi wa Tanzania John Magufuli bila hata kujali juhudi kubwa za kuleta maendeleo zinazofanywa na chama hicho.
Katibu Mkuu huiyo wa CCM ameongeza kuwa CCM haitawafumbia macho baadhi ya viongozi ambao wamekuwa na tabia aliyoiita ya kipumbavu ya kuonesha usaliti na matusi ya wazi wazi kwa Raisi Magufuli na kuongeza kuwa CCM haina mpasuko wowote isipokuwa kuna baadhi ya viongozi ndani ya chama hicho amabao hata hivyo hakuwataja majina yao kuwa ni walafi na wabinafsi na wasioitakia mema Tanzania.
Je kuna mpasuko ndani ya chama tawala?
Siku za hivi karibuni kumekuwepo na sitofahamu ndani ya CCM hadi kupelekea wadadisi wa masuala ya siasa nchini Tanzania kusema kuwa kunaonekana kuwepo na mpasuko ndani ya chama hicho.
Hali hiyoinafuatia makatibu wakuu wasitafu wa Chama cha Mapinduzi akiwemo Yusufu Makamba na Abdulrahman Kinana, kutoa waraka kwenda kwa baraza la Wazee wa chama hicho wakilalamika kuchafuliwa katika mitandao ya kijamii, na vyombo vya habari na Bwana Siprian Musiba anayejiita mwananharaki huru.
Hata hivyo wakati waraka wa makatibu wakuu hao wasitafu wa CCM ukiendelea kuzua kizungumkuti, kumekuwepo na kudukuliwa kwa sauti zinazosemekana ni za baadhii ya viongozi na wanachama wa CCM kukisika wakimtukana Rais Magufuli na kuonyesha kutokubaliana naye katika harakati zake za kuleta maendeleo nchini Tanzania.