1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

CCM yawaonya makada wake kuelekea mbio za uchaguzi

14 Julai 2022

Chama tawala nchini Tanzania, CCM kimewaonya makada wake wanaoonekana kuanza kupanga safu ya uongozi kuelekea katika uchaguzi mkuu ujao wa 2025, kikisema hakitasita kuwashughulikia ikiwamo kuwakata.

https://p.dw.com/p/4E940
Tansania CCM-Generalsekretär Amtsübergabe Abdurahman Kinana & Bashiru Ally
Picha: DW/E. Boniface

Hata hivyo, maswali yanayojitokeza ni kwa nini chama hicho kimekuwa na hulka ya kuwaonya makada wake hasa inapokaribia wakati wa uchaguzi mkuu.

Makada wa chama hicho wakubwa kwa wadogo wakati huu wanaendelea kupigana vikumbo kuelekea katika uchaguzi wa ndani ya chama ambao wanawania nafasi za wilaya, mikoa na mikutano ya taifa uchaguzi ambao umepangwa kufanyika baadaye mwaka huu.

Lakini huenda chama hicho kimeanza kunusa harufu ya vigogo wake kuanza kujiimarisha wakilenga uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.

Kufuatia hatua hiyo katibu mkuu wa chama hicho Daniel Chongolo amewanyoshea kidole akitaka wachunge nyenendo zao.

Mwaka 2025 ndio mwaka chama hicho kinataraji kufanya uchaguzi na kitaamua kuchagua makada wapya ama kusalia waliopo endapo wamefanya kwa mujibu wa ilani ya chama hicho.

Soma piaBernard Membe arejea CCM:

"Kuna watu wameanza kutafuta wapambe ili wawasaidie kwa baadae,tunawajua,tunawaona mnayoyafanya tunayajua" Alisema Chongolo.

Ingawa CCM ni chama kikongwe kinachojinasibu kuzijua vyema siasa za ndani na nje, hata hivyo wakati wote kinajikuta kikilazimika kutumia nguvu ya ziada kuwatisha makada wake wanaoonekana kujiandalia mazingira ya kabla ya uchaguzi.

Wachambuzi: Ni mbinu za kisiasa kufuta makundi ndani ya chama

Imekuwa ni jambo la kawaida kwa makada hao kuanza kampeni za chini kwa chini za mapema na mara zote uchaguzi ndani ya chama huwa ni karata ya kipekee kwa makada hao kupanga safu zinazotumika wakati wa uchaguzi mkuu kuanzia ngazi ya ubunge na urais.

Tansania CCM-Anhänger
Mfuasi wa chama tawala Tanzania CCM akishangilia Picha: DW/E. Boniface

Baadhi ya wachambuzi wa mambo wanasema, CCM tayari imepima na kubaini kile kinachoweza kujitokeza mbele ya safari, hasa kutokana na kile kinachotajwa uwezekano wa kuibuka kundi linalotaka kumpinga mwenyekiti wa sasa kutowania nafasi ya urais katika uchaguzi ujao.

Eric Bernad ni mchambuzi anayezifuatilia kwa karibu siasa za CCM ameiambia DW kwamba ni sehemu ya mkakati wa ndani wa chama hicho tawala katika kufuta kile kinachoitwa makundi ndani ya chama ambayo yatajitokeza kumpinga anaetetea nafasi husika.
Soma pia:Rais Samia ataka chama cha CCM kuendana na mabadiliko

"Hii ni mbinu ya kuondoa makundi ambayo hayatamuunga mkono mwenyekiti wa CCM" alisema Eric mfuatiliaji wa siasa ndani ya CCM.

Ingawa haijawa dhahiri, lakini kumekuwa na viashirio kwamba baadhi ya makundi ndani ya chama hicho tawala yamekuwa yakijitafakari namna kuingia katika uchaguzi huo ujao.