CDU chashinda uchaguzi wa bunge wa jimbo la Hesse
19 Januari 2009Chama cha Kansela Angela Merkel nchini Ujerumani cha Christian Democratic CDU kimepata ushindi katika uchaguzi wa jimbo la Hesse.
Katika uchaguzi huo muhimu chama hicho kimejishindia asilimia 37 ya kura takriban zote Baada ya ushindi huo waziri mkuu wa jimbo hilo Roland Koch anayeongoza chama hicho kwenye jimbo la Hesse amesema kwamba anamatumaini ya kufikia makubaliano ya kuunda serikali ya muungano na washirika wao wa chama cha FDP.
Matokeo hayo ya uchaguzi uliofanyika jana yameonyesha kwamba wahafidhina wamefanya vizuri zaidi kuliko ilivyokuwa katika uchaguzi wa mwaka jana huku chama cha Social Demokratic SPD kikishuka umaarufu ambapo kilipata asilimia 24.
Chama hicho kimeshuka kwa pointi asilimia 13 ikilinganishwa na mwaka jana Miongoni mwa vyama vidogo chama cha fdp kimejizolea asilimia 16 ya kura huku chama cha kijani the Greens wakiwa na asilimia 14 na mrengo wa shoto wakizoa asilimia 5.
Uchaguzi huo wa bunge uliotakiwa kufanyika miaka mitatu ijayo uliiitishwa mapema kufuatia mvutano wa kisiasa uliosababishwa na uchaguzi uliopita ambapo vyama vyote vikuu vilishindwa kupata wingi bungeni wa kuunda serikali.