1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Chadema kuwasajili wanachama wake kidijitali

Veronica Natalis27 Mei 2021

Chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania, Chadema kimesema kinabadili mfumo wake wa kuendesha siasa, kikilenga kuanzisha operesheni maalumu iliyopewa jina la  opereshini haki ili kukirejesha chama hicho kwa wananchi.

https://p.dw.com/p/3u3mQ
Tansania Wahlen | Treffen der Chadema-Delegierten in Dar es Salaam
Picha: DW/S. Khamis

Mwenyekiti wa chama hicho Freeman Mbowe ambaye amekuwa akifanya mikutano ya ndani, anasema operesheni hiyo inafanyika nchi nzima na moja ya mikakati yake ni kufanya siasa zisizo za kiharakati ili kupata uungwaji mkono mpya kutoka kwa wananchi wa ngazi ya chini.

Uzinduzi wa opareshini hiyo umefanyika rasmi katika makao makuu ya kanda ya kaskazini Arusha Tanzania. Chama hicho chenye wanachama hai zaidi ya milioni 10 kwa sasa, kimesema pamoja na mambo mengine  kuanzishwa kwa Oparesheni hiyo inayotarajiwa kuanza rasmi Ijumaa, katika maeneo yote ya Tanzania kumetokana na manyanyaso makubwa ya ukandamizwaji wa Demokrasia, ambao wamesema yalishuhudiwa kwa kipindi cha zaidi ya muongo mmoja sasa.

Chadema chataka wabunge wake waloapishwa kujieleza

Opareseheni hiyo ya kidijitali iliyo na kauli mbiu ya "Tunakwenda Kidijitali” itahusisha kuandikisha wanachama upya kabisa na kutolewa kwa kadi za kielekroniki, ambazo zitakuwa katika makundi matano kulingana na kiwango cha pesa kitakachotolewa na wanachama. Mbali na kuimarisha misingi ya uchumi ndani ya chama, lakini pia Chadema inamatumaini ya kujijenga na kupata wafuasi wapya hasa vijana.

Mbali na uzinduzi wa Oparesheni hiyo, Chama hicho pia kimesema kinaanza rasmi mchakato wa kudai katiba mpya, tume huru ya uchaguzi na uimarishwaji wa misingi ya utawala unaozingatia sheria, kikisema kuwa hakitashiriki uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 kama masuala hayo hayatatekelezwa.