1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

CHADEMA yaamua kuanza mikutano ya hadhara

16 Machi 2020

Siku chache baada ya kutolewa jela viongozi wake wakuu, chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania, CHADEMA, kinasema sasa kitaanza mikutano ya hadhara nchi nzima kudai tume huru ya uchaguzi kwa mujibu wa sheria.

https://p.dw.com/p/3ZWZK
Freeman Mbowe
Picha: DW/S. Khamis

Akizungumza na waandishi wa habari kwenye makao makuu ya chama chake jijini Dar es Salaam, mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe,  ametangaza kufika ukomo wa kile alichokiita "subira ya kutofanya mikutano ya kisiasa kwa takribani miaka minne sasa" na hivyo wataanza kufanya mikutano ya hadhara kuanzia mwezi wa Aprili "kudai tume huru ya uchaguzi pamoja na maandalizi ya kuelekea uchaguzi wa Oktoba 2020."

Hata hivyo, bado Mbowe alionekana kunyoosha mkono wa maridhiano akiutaka utawala wa nchi kuchukuwa hatua za kabla ili kusaka maridhiano ya kisiasa, kabla chama chake hakijaanza rasmi kuchukuwa hatua hiyo.

"Yawezekana upole wa Watanzania kwa miaka hii minne, kukubali maelekezo yaliyo kinyume cha katiba na sheria na nchi, tumeonekana Watanzania wote ni wajinga. Tumekuwa waungwana sana kutafuta maridhiano ili tusiingize nchi kwenye machafuko," alisema mwenyekiti huyo wa CHADEMA, ambaye alitoka jela siku ya Jumamosi baada ya kulipia fedha za faini shilingi milioni 70 za Kitanzania.

Chadema leaders Halima Mdee, Ester Matiko und Ester Bulaya
Wabunge watatu wanawake wa chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania, ambao walikuwa wamefungwa jela: kutoka kushoto Ester Matuko, Esther Bulaya na Halima Mdee.Picha: DW/E. Boniphace

Mbowe na wenzake zaidi ya sita - wote wakiwa viongozi wa ngazi za juu wa chama hicho kikuu cha upinzani - walikuwa wamehukumiwa aidha kulipa faini ya shilingi milioni 350 ama kwenda jela miezi mitano kwa kila kosa katika takribani makosa 12 waliyokuwa wametiwa hatiani.

Wote walilipa faini kwa fedha zilizochangiwa kufuatia kampeni kubwa ya uhamasishaji iliyoongozwa na chama hicho ndani na nje ya nchi.

Katika hatua nyengine, Mbowe amewaambia waandishi wa habari kwamba tukio la kushambuliwa na kuwekwa ndani kwa wafuasi na viongozi wake mwishoni mwa wiki wakiwa kwenye gereza la Segerea lilikuwa la makusudi na kimkakati lililofanywa na askari magereza mwishoni mwa juma lililopita.

Katika tukio hilo, wabunge watatu wanawake - Esther Bulaya, Halima Mdee na Jesca Kishoa - walidaiwa kupigwa na kujeruhiwa vibaya na askari magereza, wakiwa sehemu ya viongozi na wafuasi wa CHADEMA walijitokeza kwenda kumlaki Mbowe kutoka gerezani.

Hawa Bihoga, DW Dar es Salaam