1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Chadema yaikosoa serikali kwa kuwatesa viongozi wake

14 Agosti 2024

Chama Kikuu cha Upinzani Tanzania Chadema kimeishutumu vikali serikali baada ya viongozi wa chama hicho kudaiwa kupigwa, kuteswa na kuwekwa mahabusu.

https://p.dw.com/p/4jT0j
Naibu mwenyekiti wa chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania, Tundu Lissu
Naibu mwenyekiti wa chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania, Tundu LissuPicha: AP Photo/picture alliance

Viongozi hao wa Chadema, akiwamo Mwenyekiti wa kitaifa, Freeman Mbowe, Katibu Mkuu John John Mnyika, Makamu Mwenyekiti Tundu Lisuu na John Pambalu, wameeleza kwa kina jinsi walivyokamatwa, kuteswa na jeshi la polisi wakati wakiandaa kongamano la maadhimisho ya siku ya vijana Agosti 12, mkoani Mbeya.
 
Katika mkutano huo, Chadema wamelaani vikali kitendo cha Jeshi la Polisi kuwakamata viongozi hao na kuwatesa, kisha wakatoa azimio kuwa, jopo la wanasheria wa Chadema, wanakwenda kuwashtaki Naibu Msajili wa Vyama vya Siasa nchini,  Cyst Nyahoza kwa kuzuia kongamano hilo kinyume cha sheria na Kamishna wa Jeshi la Polisi, Awadh Haji, kwa kuongoza mashambulizi dhidi ya viongozi hao.

Viongozi wa chama hicho na wanachama zaidi ya 500 walikamatwa wakati wakiandaa kongamano la maadhimisho ya  Siku ya Vijana, Agosti 12 mwaka huu, mkoani Mbeya. Hata hivyo, siku moja baadaye, viongozi na baadhi ya wanachama waliachiwa kwa dhamana.
 
Serikali haikupaswa kuwatesa viongozi baada ya kuwakamata

Chama cha upinzani Chadema kiwasilisha mashtaka dhidi ya Mkuu wa Polisi Tanzania
Chama cha upinzani Chadema kiwasilisha mashtaka dhidi ya Mkuu wa Polisi TanzaniaPicha: Eric Boniface

Kadhalika viongozi hao wakiongozwa na Mwenyekiti Freeman Mbowe, wamelaani kitendo cha jeshi la polisi kuharibu vifaa vya kazi na simu za wanahabari wa mkoani Mbeya waliokuwa katika eneo hilo kwa ajili ya kuripoti kongamano hilo. Kwa upande wake Lissu, amesema shughuli ya Baraza la Vijana la CHADEMA ilifanyika kwa kufuata utaratibu wa kisheria lakini ilizuiwa kwa kutumia mabavu ya kijeshi. 

Mnyika, Katibu Mkuu wa chama ambaye ni mmoja kati ya waliokamatwa alitumia nafasi hiyo kueleza jinsi yeye na Mwenyekiti wa Chadema, kanda ya Nyasa, Joseph Mbilinyi, maarufu Sugu, walivyokamatwa, kuteswa na kusafirishwa kwa  karandinga la polisi kutoka Mbeya hadi Dar es Salaam huku wakiwa wamelazwa kifudifudi.  Ameeleza namna askari hao walivyowakamata wanachama wa kongamano hilo, kuwapulizia maji ya kuwasha, kuwapiga kwa shoti za umeme na kuwakanyaga.

Mwenyekiti wa Vijana wa Chadema, John Pambalu amesema vijana ndio waamuzi wa hatma ya taifa hili na akawataka waamue kupambana na kile alichokiita udhalimu unaofanywa na serikali dhidi ya wapinzani.
 
Awali, kabla ya viongozi wa chadema kukamatwa, jeshi la polisi lilipiga marufuku kongamano hilo, na marufuku hiyo ilitanguliwa na barua kutoka ofisi ya msajili wa vyama vya siasa, ikiitaka Chadema kusitisha kongamano hilo, siku ya Agosti 12.