1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Chadema yasema Lisu hakuwa salama kwa kuikosoa Serikali

Caro Robi
8 Septemba 2017

Chama kikuu cha upinzani Tanzania ambacho mwanachama wake wa ngazi ya juu Tundu Lisu alipigwa risasi takriban ishirini na tano kimesema kuwa, Lisu hakuwa salama kwa muda mrefu kutokana na kuikosoa serikali hadharani.

https://p.dw.com/p/2ja1M
Ringen um neue Verfassung in Tansania
Picha: DW/M.Khelef

Makamu mwenyekiti wa Chadema Profesa Abdallah safari amelaani vikali shambulizi hilo la risasi lililomlenga Lisu na kuongeza kuwa kutokana na sababu za kiusalama, chama pamoja na familia ya Tundu Lisu wamekataa, asitibiwe hospitali ya taifa ya Muhimbili na badala yake amepelekwa Nairobi, Kenya kwa matibabu.

Tukio la shambulio la risasi dhidi ya mwanasiasa aliejitoa mbele kuikosoa serikali hadharani Tundu lisu, limeshtua wengi ndani na nje ya Tanzania ambapo katika mitandao ya kijamii ujumbe wa kulaani shambulio hilo, pamoja na kumtakia heri mbunge wa Singida mashariki na mwanansheria mkuu wa chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania Chadema Tundu Lisu zinaendelea kumiminika.

Polisi yatakiwa kuwataja wahusika wa shambulizi

Akizungumza  kwa simanzi mbele ya waandishi wa habari, makamu mwenyekiti wa chama cha Chadema, Profesa Abdallah safari amesema, familia pamoja na chama hakikua tayari kumpeleka Tundu lisu katika hospitali ya taifa muhimbili kutokana na sababu za kiusalama, licha ya serikali kupendekeza apokee matibabu katika hospitali hiyo.

Tansania Polizeizentrale in Dar es Salaam
Jeshi la Polisi la TanzaniaPicha: DW/Said Khamis

Hata hivyo spika wa bunge la Jamhuri ya muungano wa Tanzania amewashauri, na wameridhia wabunge wote, kutoa nusu ya posho zao kwa ajili ya kuchangia matibabu ya Lisu, ambapo kiasi cha takribani shilingi za Tanzania milioni arobaini na tatu zinatarajiwa kupatikana kwa ajili ya matibabu yake.

Katibu mkuu wa Chadema dokta Vincent Mashinji, katika mkutano huo amesema kuwa, lazima jeshi la polisi lijitokeze hadharani na kuwataja  watu waliohusika na shambulizi hilo la risasi dhidi mwanansheria mkuu wa chadema. Lakini matukio ya watu kutishiwa pamoja na mashambulio mbalimbali yanashuhudiwa kwa hivi karibu nchini, kunatajwa kuwa na ulakini wa uwajibikaji wa serikali katika kuwalinda wananchi wake ipasavyo.

Waziri mkuu mstaafu wa awamu ya tatu Fredrick sumaye anasema, bado serikali inatakiwa iwajibike kutokana na ishara ya matukio ya aina hii. Punde baada ya kumalizika mkutano huo wanachama wamepaaza sauti wakisema kwa ghadhabu kuwa, hayo ni maneno mepesi yanayotoka kwa viongozi wao.

Mwandishi: Hawa Bihoga

Mhariri: Saumu Yusuf