Chakwera aapishwa rais mpya nchini Malawi
28 Juni 2020Kiongozi wa upinzani nchini Malawi Lazarus Chakwera ameapishwa kuingia madarakani leo Jumapili na kuwa rais mpya wa nchi hiyo,baada ya kushinda katika marudio ya uchaguzi mkuu.
Chakwera alipata ushindi wa asilimia 58.57 ya kura zote. Sherehe ya kumuapisha rais huyo mpya imefanyika katika mji mkuu wa Malawi Lilongwe. Katika hotuba yake aliyotoa baada ya kuapishwa amewashukuru Wamalawi akisema wamempa heshima kubwa iliyompa furaha isiyokuwa na kifani.
Rais Chakwera ameongeza kuwaambia wananchi wa Malawi kwamba heshima walioonesha imetokana na nia na kiu chao cha kutaka mabadiliko.
Wamalawi wameamua
Kiasi ya wapiga kura milioni 6.8 katika taifa hilo dogo la kusini mwa Afrika walijitokeza katika vituo vya kupigia kura siku ya Junanne. Na jana Jumamosi , tume ya mwenyekiti wa tume ya uchaguzi Chifundo Kachale aliwaambia waandishi habari; "Tume imemtangaza Lazarus Chakwera , kwa kupata asilimia 58.57 ya kura, kuwa amechaguliwa kuwa rais wa Malawi.
Mutharika alikuwa wa pili kwa kupata kura 1,751,377, wakati mgombea ambaye hajulikani sana Peter Dominico Kuwani amepata kuwa 32,456.
Watu waliojitokeza kupiga kura ni asilimia 64.81.
Shangwe ushindi wa Chakwera
Tangazo hilo lilipokelewa kwa shangwe kubwa na vigelegele wakati waungaji mkono upinzani wakipepea bendera ya Malawi yenye rangi nyekundu , nyeusi na kijani na kuimba "serikali" katika lugha ya Kichechewa.
Mwezi Februari , mahakama ya juu ya Malawi iliona kuwa uchaguzi wa kwanza umegubikwa na mapungufu mengi , ikiwa ni pamoja na matumizi ya wino wa kufanyia marekebisho kubadilisha matokeo katika karatasi ya matokeo.
Hukumu hiyo ya kihistoria imeifanya Malawi kuwa nchi ya pili ya Afrika kusini mwa jangwa la Sahara kubatilisha matokeo ya rais , baada ya Kenya mwaka 2017.
Rais Mutharika anayeondoka madarakani wa chama cha Democratic Progressive Party DPP siku ya Ijumaa alitoa wito kwa tume ya uchaguzi ya Malawi kubatilisha matokeo ya kura ya pili na itangaze uchaguzi wa tatu.
Mwandishi: Saumu Mwasimba
Mhariri:Tatu Karema