Chama cha ANC kiko tayari kwa serikali ya Umoja wa Kitaifa
7 Juni 2024Rais wa nchi hiyo ambaye pia ni mwenyekiti wa chama cha ANC Cyril Ramaphosa amewaambia waandishi habari baada ya kuwa na mkutano na uongozi wa chama hicho jana jioni,kwamba wamekubaliana kuvialika vyama vyote katika mchakato wa kuunda serikali ya Umoja wa Kitaifa.
Ramaphosa amesema hatua hiyo ndiyo bora zaidi ya kuifanya nchi hiyo kusonga mbele.
Pendekezo hilo la ANC linamaanisha Afrika Kusini inataka kuwa na serikali ya mseto itakayojumuisha vyama vyote vilivyopata viti katika bunge la nchi hiyo wakati wa uchaguzi.
Soma pia: Chama cha ANC chasaka kuunda serikali ya umoja wa kitaifa
Chama hicho kimesema serikali ya Umoja wa Kitaifa itawakilisha maslahi ya wapiga kura wote.
Wachambuzi lakini wana wasiwasi kwamba serikali ya Umoja wa Kitaifa huenda ikashindwa kupata uthabiti wa taifa na kushindwa kufikia makubaliano.