Chama cha upinzani Myanmar chashinda kwa kishindo
9 Novemba 2015Kulingana na msemaji wa chama cha National League for Democracy NLD,Win Htein chama hicho cha upinzani kimejinyakulia viti vya kutosha kukiwezesha kuunda serikali ijayo.
Htein amesema chama cha NLD kimekusanya matokeo kutoka vituo vya kupigia kura kote nchini humo yanayoashiria kuwa kinashinda kwa zaidi ya asilimia tisini katika eneo la kati ya nchi hiyo.
NLD chashinda Yangon
Tume ya uchaguzi ya Myanmar imeanza kutangaza matokeo ya jimbo hadi jimbo na chama cha NLD kimeshinda viti vyote 12 vya bunge katika mji mkubwa zaidi nchini humo-Yangon. Na kati ya viti kumi na sita vilivyotangazwa na tume nchini humo NLD kimejishindia viti 15. Chama cha Suu Kyi ambaye ni mshindi wa tuzo ya amani ya Nobel kimeshinda kwa zaidi ya asilimia 65 ya kura zilizopigwa katika majimbo ya Mon na Kayin.
Chama tawala cha Myanmar cha Union Solidarity and Development USDP kimekubali kushindwa katika uchaguzi huo. Kaimu mwenyekiti wa USDP Htay OO ameliambia shirika la habari la Reuters kuwa wameshindwa katika uchaguzi huo wa kwanza huru nchini humo katika kipindi cha robo karne.
Uchaguzi huo ni wa kihistoria katika taifa hilo ambalo limekuwa katika safari ya panda shuka tangu miaka ya sitini kuelekea kufikia na kuzingatia demokrasia kutoka utawala wa kiimla wa kijeshi ambao umelifanya taifa hilo kutengwa kwa muda mrefu.
Hata hivyo licha ya matokeo ya uchaguzi yatakavyokwenda, Myanmar inaelekea katika kipindi cha sintofahamu kuhusu ni jinsi gani Suu Kyi na vyama vingine vitajadili suala la kugawana madaraka katika taifa ambalo bado jeshi lina ushawishi mkubwa.
Hata kama chama chake kitashinda wingi wa viti kukiwezesha kuunda serikali ijayo, Suu Kyi amezuiwa kikatiba kuingia madarakani kama Rais. Kiongozi huyo amesema atakuwa na ushawishi mkubwa kwa rais mpya licha ya kuwa katiba haimruhusu yeye kuwa kiongozi wa Myanmar na kuitaja katiba hiyo kuwa ya 'kipuuzi sana'.
Jeshi lina ushawishi mkubwa
Jeshi ndilo liliifanyia marekebisho katiba kwa maslahi yake na kumzuia Suu Kyi kuitawala Myanmar. Kuambatana na katiba hiyo robo ya viti vya bunge vitapewa wanachama wa jeshi ambao hawatachaguliwa na raia.
Jeshi pia linapewa mamlaka na katiba kuchukua madaraka kutoka kwa serikali katika mazingira fulani, kupewa nyadhifa katika baraza la mawaziri na kuudhibiti uchumi.
Maafisa wa tume ya uchaguzi wanatarajiwa kufanya mkutano na wanahabari baadaye leo jioni ambapo matokeo zaidi yatatolewa huku matokeo kamili yakitarajiwa katika kipindi cha siku kumi zijazo.
Rais Thein Sein na mkuu wa jeshi la Myanmar wameahidi kuheshimu matokeo ya uchaguzi huo hata kama chama tawala USDP kinachoungwa mkono na jeshi kitashindwa.
Mwandishi: Caro Robi/Reuters/ap
Mhariri:Yusuf Saumu