1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Chama cha Suu Kyi kuunda serikali Myanmar

13 Novemba 2015

Chama cha upinzani Myanmar cha National League for Democracy-NLD kimeshinda viti vya kutosha bungeni kukiwezesha kumchagua Rais na kuunda serikali ijayo.

https://p.dw.com/p/1H4yg
Myanmar Parlamentswahl Sieg Aung San Suu Kyi
Picha: Reuters/J. Silva

Tume ya uchaguzi ya Myanmar imetangaza hii leo kuwa chama hicho cha upinzani kinachoongozwa na Aung San Suu Kyi kimeshinda viti vingine zaidi katika mabunge yote mawili nchini humo katika uchaguzi mkuu uliofanyika Jumapili iliyopita na hivyo kupitisha idadi ya viti 329 vinavyohitajika kukiwezesha kumchagua Rais.

Ushindi huo mkubwa wa NLD unamaanisha kuwa chama hicho kinaweza kuwateua wawili kati ya wagombea watatu wa wadhifa wa rais licha ya kuwa Suu Kyi mwenye umri wa miaka 70 anazuiwa na katiba ya nchi hiyo kuwa Rais kwa sababu wanawe wana uraia wa kigeni.

Chama hicho cha upinzani kinachosimamia misingi ya demokrasia kinayo fursa ya kuuondoa utawala unaoungwa mkono na jeshi la Myanmar na kuipa nafasi demokrasia na mageuzi ya kiuchumi.

Ukurasa mpya Myanmar

Baada ya zaidi ya miongo mitano ya utawala wa kijeshi nchini Myanmar, Suu Kyi, mshindi wa tuzo ya amani ya Nobel ambaye leo anatimiza miaka mitano tangu kuachiwa na jeshi kutoka kifungo cha nyumbani anatarajiwa kuibadilisha sura ya kisiasa kwa kuwa na usemi mkubwa katika serikali ijayo.

Kiongozi wa upinzani Myanmar Aung Suu Kyi
Kiongozi wa upinzani Myanmar Aung Suu KyiPicha: Reuters/C. McNaughton

Lakini wachambuzi wanasema ushindi wa NLD sio mwisho wa ushawishi wa jeshi la Myanmar kwani katiba inalihakikishia robo ya viti bungeni na nyadhifa muhimu katika baraza la mawaziri na za usalama na ulinzi.

Rais Thein Sein ambaye chama chake cha Union Solidarity and Development USDP kimeshindwa vibaya na mkuu wa majeshi Min Aung Hlaing wamekipongeza chama cha NLD kwa ushindi wake na wameahidi kuyaheshimu matokeo ya uchaguzi huo na kusaidia kuhakikisha kipindi cha mpito cha kukabidhi madaraka kitaendeshwa kwa amani.

Awali Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon alimpongeza Suu Kyi baada ya chama chake kushinda kwa kishindo katika uchaguzi mkuu lakini ameonya bado kuna kazi kubwa mbele ya kujenga demokrasia Myanmar.

Ban ameutaja uchaguzi huo wa kihistoria kama hatua muhimu katika mchakato wa taifa hilo kuondokana na mfumo wa utawala unaodhibitiwa na jeshi.

Jumuiya ya kimataifa yampongeza Suu Kyi

Hata hivyo amesikitika kuwa jamii ya walio wachache ya Rohingya haikuruhusiwa kushiriki katika uchaguzi huo. Ban ameahidi Umoja wa Mataifa utaisaidia Myanmar ambayo ilikuwa imetengwa kwa muda mrefu na jumuiya ya kimataifa, kujiimarisha kidemokrasia na kuheshimu haki za binadamu.

Katbu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon na Rais wa Marekani Barack Obama
Katbu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon na Rais wa Marekani Barack ObamaPicha: picture alliance / landov

Wakati huo huo, Rais wa Marekani Barack Obama amempigia simu Suu Kyi kumpongeza na kumsifu kwa juhudi zake za kujitolea kwa miaka mingi kuendeleza amani na demokrasia Myanmar.

Ban na Obama pia wamempongeza Rais Sein kwa kuandaa kwa ufanisi mkubwa uchaguzi huo wa kihistoria. Ban amemsifu Sein kwa ujasiri na maono yake katika uchaguzi huo.

Marekani imesema inatafakari kuiondolea Myanmar baadhi ya vikwazo ilivyokuwa imeiwekea. Uchaguzi huo wa kwanza kwa chama cha NLD kujitosa tangu mwaka 1990, umeshuhudia idadi kubwa ya wapiga kura waliojitokeza kukipa ushindi wa zaidi ya asilimia 80.

Mwandishi: Caro Robi/dpa/afp/reuters

Mhariri:Josephat Charo