1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Chile wanyakua Kombe la Copa America

6 Julai 2015

Chile ndio mabingwa wa Kombe la Mataifa ya Amerika Kusini – Copa America 2015, baada ya kuwapiku Argentina kupitia kwa mikwaju ya penalti 4-1. Hii ni baada ya mchuano kukamilika 0-0

https://p.dw.com/p/1FtAJ
Fußball Copa America Chile Argentinien Vargas
Picha: AP

Wenyeji Chile walikuwa na kila sababu ya kusherehekea kwa sababu ilikuwa ni mara ya kwanza kwao kushinda Kombe la Copa America tangu lilipoanzishwa miaka 99 iliyopita.

Argentina sasa itaendelea kujiuliza maswali ni kwa nini mambo yanawaendea mrama maana ni miaka 22 tangu washinde kombe lolote kubwa kwenye mashindano ya kandanda ya kimataifa.

Mchezaji wa Arsenal Alexis Sanchez alifunga penalti ya ustadi na ya ushindi baada ya mshambuliaji wa Argentina Gonzalo Higuain kupiga nje penalti yake huku mkwaju wa Ever Banega ukipanguliwa na mlinda mlango mahiri Claudio Bravo. Bravo alishinda tuzo ya kipa bora wa dimba hilo. Miongoni mwa maelfu ya mashabiki waliojaa kuishabikia timu yao ni wachimba mgodi 33 waliokwama chini ya mgodi kwa wiki kadhaa mwaka 2010, katika kisa kilichovutia hisia nyingi duniani.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP
Mhariri: Josephat Charo