China kutoa chanjo ya Covid-19 kwa nchi 40 za Afrika
20 Mei 2021
Afisa mmoja wa wizara ya mambo ya nje ya China amewaambia waandishi wa habari leo Alhamisi kuwa dozi hizo za chanjo ya Covid-19 zinazopelekwa katika nchi Afrika ama zimetolewa bure au zimeuzwa kwa bei nafuu. Afisa huyo, Wu Peng amelinganisha kitendo hicho cha China na misimamo ya baadhi ya nchi ambazo hakuzitaja, ya kusubiri hadi pale raia wake wote watakapokuwa wamepata chanjo kabla ya kuruhusu chanjo wanazotengeneza kusafirishwa katika mataifa mengine. Inadhaniwa kuwa bila shaka alikuwa akiipiga kijembe Marekani.
Wu amesema ingawa China pia inaamini kuwa ni lazima raia wake wapate chanjo haraka iwezekanavyo, haifumbia macho mahitaji katika nchi nyingine na inafanya iwezavyo kutoa msaada.
Kupaza sauti ya Afrika
Afisa huyo ambaye anaongoza kitengo cha Afrika katika wizara ya mambo ya nje ya China, ameitolea mwito jumuiya ya kimataifa kufuata mfano wa nchi yake.
''Sio tu tunaihimiza jumuiya ya kimataifa na mataifa yenye uwezo kutoa chanjo zaidi kwa Afrika, bali pia tunaunga mkono rai ya nchi za Kiafrika kutaka sera za upendeleo kwa bara hilo, katika ubadilishanaji wa teknolojia na kuondoa hatimiliki linapohusika suala la chanjo.'' Amesema Wu.
Wakati Marekani ikishutumiwa kujilimbikizia dozi za chanjo ya Covid-19, rais wa nchi hiyo Joe Biden Jumatatu wiki hii aliahidi kutoa dozi milioni 20 kwa nchi nyingine katika muda wa wiki sita zijazo, kiwango hicho kikifikisha msaada wa chanjo wa Marekani kwenye dozi milioni 80. Utawala wa Biden haukuweka bayana nchi zitakazonufaika na msaada huo.
Marekani pia yajitolea
Shehena hiyo mpya kutoka Marekani itahusisha chanjo zilizotengenezwa na makampuni ya Kimarekani ya Pfizer, Moderna au Johnson&Johnson. Aidha, siku za nyuma utawala wa Rais Biden ulikuwa umeahidi kutoa dozi milioni 60 za chanjo inayotengenezwa na AstraZeneca ifikapo mwishoni mwa mwezi ujao wa Juni.
Hapo jana Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilitaka kasi ya upatikanaji wa chanjo barani Afrika iongezwe, likielezea wasiwasi juu ya ukweli kuwa Afrika imepata asilimia 2 tu ya chanjo za Covid-19 zilizokwishasambazwa kote duniani.
China imekuwa ikipata mafanikio makubwa katika kile kilichopachikwa jina la 'diplomasia ya chanjo', kwani tayari imekwishajitolea kuzisaidia nchi 45 kwa dozi zaidi ya milioni 500, hii ikiwa ni kwa mujibu wa takwimu zilizokusanywa na shirika la habari la Associated press.
ape, rtre