1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaSerbia

China na Serbia zatia saini makubaliano ya pamoja

8 Mei 2024

China na Serbia zimetia saini makubaliano ya kujenga "mustakabali wa pamoja" wakati wa ziara ya Rais Xi Jinping nchini Serbia na kuifanya nchi hiyo kuwa ya kwanza Ulaya kuingia katika makubaliano kama hayo na China

https://p.dw.com/p/4fddo
Rais wa China Xi Jinping ampokea Rais wa Serbia Vucic mjini Beijing, Oktoba 17, 2023
Rais wa China Xi Jinping (Kulia) akutana na mwenzake wa Serbia Aleksandar Vucic (kushoto)Picha: Yan Yan/Xinhua/picture alliance

Baada ya kukutana mjini Belgrade, Xi na mwenzake wa Serbia, Aleksandar Vucic, walitangaza kuimarisha ushirikiano wa kimkakati kati ya mataifa hayo mawili na kujenga enzi mpya ya jamii yenye mustakabali wa pamoja kati yao.

Soma pia:Xi awasili Serbia kituo cha pili cha ziara yake Ulaya

Wakati wa mkutano kati ya viongozi hao wawili, Xi alisema  kwamba wakati wa ziara yake ya mwisho nchini Serbia, waliamua kwa pamoja kuimarisha uhusiano wao kufikia ushirikiano mkubwa wa kimkakati.

Serbia ni mshirika wa kwanza wa kimkakati wa China

Xi ameongeza kuwa tangu wakati huo, Serbia imekuwa mshirika wa kwanza wa kimkakati wa China katika Ulaya ya Kati na Mashariki.

Kwa upande wake, Rais Vucic alihutubia umati wa watu akiwa kwenye roshani akimuita Rais Xi rafiki wa dhati.

Vucic aitaja ziara ya Xi kuwa ya kihistoria

Vucic alisema kuwa ziara ya Xi nchini Serbia ilikuwa ya "kihistoria" kwa sababu imefungua njia ya mahusiano ya karibu zaidi huku akisema kwamba wanaandika historia ijapokuwa haionekani hivyo kwa wengi.

Soma pia: Xi: China ´isichafuliwe jina´ kutokana na mzozo wa Ukraine

Rais huyo wa Serbia alimshukuru Xi akielezea kuwa kiongozi huyo wa China hajafanya ziara barani Ulaya kwa muda wa miaka mitano na wakati wa ziara yake ya sasa, ameichagua tena kufika nchini humo.

Mnamo mwaka 2016, nchi hizo mbili zilitia saini makubaliano ya ushirikiano wa kimkakati na mwaka jana, zikaingia kwenye makubaliano ya biashara huria.

Mchakato wa Serbia wakujiunga na Umoja wa Ulaya umekuwa ukiyumba

Baadhi ya makubaliano kati ya China na Serbia, kama vile mkataba wa biashara huria, hayaambatani na masharti ya uanachama wa Umoja wa Ulaya. Ijapokuwa Serbia inataka kujiunga rasmi na Umoja huo wa mataifa 27, imekuwa ikiyumba katika mchakato huo.

Haikubainika wazi mara moja jinsi Umoja wa Ulaya utakavyojibu hatua ya Serbia ya kukaribiana zaidi na China.

Soma pia:Macron: China itumie ushawishi wake kusitisha vita Ukraine

Vita vya Urusi nchini Ukraine vimesababisha kujumuishwa kwa mataifa sita ya eneo la Balkan ikiwa ni pamoja na Serbia kuwa katika kilele cha ajenda ya Umoja wa Ulaya.

Rais wa halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen akihutubia wanahabari mjini Paris mnamo Mei 6, 2024
Rais wa halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya Ursula von der LeyenPicha: Dimitar Dilkoff/AFP

China imekataa kuita shambulizi la Urusi nchini Ukraine kuwa uvamizi

China inadai kutoegemea upande wowote katika mzozo huo wa Ukraine, lakini imekataa kuliita shambulio la Urusi kuwa uvamizi na pia imeshutumiwa kwa kuimarisha uwezo wa kijeshi wa nchi hiyo.

Soma pia:Rais Xi wa China akosoa NATO kabla ya ziara yake ya Serbia

Serbia nayo imelaani uvamizi wa Urusi nchini Ukraine lakini imekataa kujiunga katika vikwazo vya kimataifa dhidi ya Urusi.

Baadaye leo, Xi atasafiri kuelekea Hungary. Kama vile Serbia, Hungary inaonekana kuwa mmoja wa washirika wa karibu wa China barani Ulaya.