1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

China na Urusi zazuia vikwazo dhidi ya Korea Kaskazini

21 Januari 2022

China na Urusi zimezuia shinikizo la Marekani kuwawekea vikwazo raia watano wa Korea Kaskazini kama jawabu la Korea Kaskazini kurusha makombora ya masafa marefu hivi karibuni. 

https://p.dw.com/p/45s9U
Russland Nordkorea l Treffen von  Vladimir Putin und Kim Jong Un
Picha: picture-alliance/AP/A. Young-Joon

Hatua hii ya China inakuja kabla kufanyika kwa mkutano wa faragha wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusiana na Korea Kaskazini ulioitishwa na Marekani. Urusi nayo imeifuata China katika kulipinga pendekezo la Marekani.

China na Urusi zote kwa muda mrefu zimepinga Korea Kaskazini kuongezewa shinikizo na walikwenda hata hatua ya kutaka iondolewe vikwazo vya kimataifa kwa ajili sababu za kiutu.

Baada ya Marekani wiki iliyopita kuwawekea vikwazo raia watano wa Korea Kaskazini wanaohusishwa na mpango wa makombora ya masafa marefu ya nchi hiyo, iliendeleza kampeni katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lenye wanachama 15 ili watu hao waongezewe vikwazo vya Umoja wa Mataifa pia.

Wizara ya fedha ya Marekani inasema mmoja wa raia hao wa Korea Kaskazini Choe Myong Hyon ana makao nchini Urusi. Na sasa Marekani imeelezea kutoridhishwa kwake na kuzuiwa kwa hatua hiyo ya kutowawekea vikwazo.

Linda Thomas-Greenfield ni balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa.

USA I US Botschafterin Linda Thomas-Greenfield I UN
Linda Thomas-Greenfield balozi wa Marekani Umoja wa MataifaPicha: Luiz Rampelotto/EuropaNewswire/picture alliance

"Ni muhimu sana kwa mataifa wanachama kuchukua hatua za kuviweka vikwazo hivyo kutokana na uwezo wao au kuwepo na hatari ya kuipa Korea Kaskazini uhuru wa kuuendeleza mpango wake wa silaha."

Chini ya sheria za sasa za Umoja wa Mataifa, kuzuiwa kwa vikwazo hivyo kunadumu kwa kipindi cha miezi sita na baada ya hapo mwanachama mwengine wa Baraza la Usalama anaweza kuongeza muda huo kwa miezi mitatu zaidi na siku moja kabla pendekezo hilo halijaondolewa kabisa kutoka kwenye meza ya mazungumzo.

Kulingana na Greenfield, mkutano wa hapo jana wa Baraza la Usalama kuhusu Korea Kaskazini ambao ni wa pili katika siku kumi na moja, ulikuwa ni kwa ajili ya kujadili jawabu kwa majaribio ya makombora yaliyofanywa hivi karibuni.

Ujumbe wa kidiplomasia wa China kwa Umoja wa Mataifa pamoja na Urusi hawakutoa jawabu lolote walipoulizwa kuhusiana na suala hilo. Korea Kaskazini imefanya msururu wa majaribio ya makombora ikisema ni haki yake ya kisheria kujilinda.