China yaonya juu ya kuporomoka biashara duniani
16 Januari 2024Waziri Mkuu wa China, Li Qiang, aliwaambia wanasiasa na wafanyabiashara wanaokusanyika kwenye kongamano hilo la 54 la uchumi duniani kwamba vigingi vya kibaguzi vya biashara ni kitisho kwa uchumi wa ulimwengu.
Bila kuitaja Marekani kwa jina, waziri mkuu huyo wa China alisema hatua mpya zinazochukuliwa zina madhara ya moja kwa moja kwa uwekezaji na zinaweza haraka sana kuuziba pumzi uchumi wa dunia nzima.
"Kwenye dunia ya leo, nchi zina maingiliano makubwa ya kiuchumi, jambo linalomaanisha kwamba sera zao za uchumi zina athari inayofika mbali na kwa haraka. Kutokana na migogoro inayoukumba ulimwengu na hatua zinazotafautiana kukabiliana nayo zitaufanya uchumi wa dunia kuwa mashakani zaidi. Linalopaswa kufanyika ni kushirikiana katika mazingira ya uwazi, ya haki na yasiyo ya kibaguzi kwa maendeleo ya sayansi na teknolojia na kuondosha vikwazo vinavyotatiza usambazaji wa ubunifu ili ubunifu ushamiri." Alisema Qiang.
Soma zaidi: Jukwaa la Uchumi Duniani la Davos kuanza leo
Mizozo ya kibiashara kati ya China na Marekani ilishamiri wakati wa utawala wa Donald Trump, na imeendelea kuwapo chini ya utawala wa Joe Biden. Mnamo mwezi Oktoba, Marekani ilitangaza vikwazo vipya kwa vifaa vya teknolojia ya akili bandia, hatua iliyoighadhabisha sana China.
Zelenksy asaka misaada Davos
Kwa upande wake, Rais Volodymyr Zelensky wa Ukraine yuko Davos kusaka misaada zaidi na uungaji mkono wa kimataifa kwa nchi yake inayokabiliana na uvamizi wa Urusi kwa mwaka wa pili sasa, wakati huu makini ya ulimwengu ikielekezwa kwenye vita vya Israel katika Ukanda wa Gaza.
Katika hotuba yake kwenye mkutano huo, Rais wa Kamisheni ya Umoja wa Ulaya, Ursula von der Leyen, alirejelea msimamo wa Umoja huo kuendelea kuisaidia Ukraine hadi ishinde vita vyake na Urusi.
Soma zaidi: Urusi yasema mazungumzo ya DAVOS hayatafanikiwa
"Ukraine inaweza kushinda kwenye vita hivi, lakini lazima tuendelee kuiwezesha kwenye mapambano yake. Watu wa Ukraine wanahitahi kuwa na ufadhili wa kifedha unaotabirika ndani ya mwaka mzima wa 2024 na hata baada ya hapo. Wanahitaji msaada wa uhakika wa silaha kuilinda ndhi yao na kurejesha mamlaka yao. Wanahitaji kuwa na uwezo wa kuzuwia mashambulizi ya Urusi ya siku zijazo." Alisema von der Leyen.
Kwa upande wake, Mkuu wa Kampuni ya DP World ya Dubai aliuambia, Yuvraj Narayan, aliwaambia washiriki wa mkutano huo kwamba kinachoendelea kwenye Bahari ya Shamu, ambako meli za mizigo zinazuiwa kupita kutokana na mashambulizi ya waasi wa Kihouthi nchini Yemen, kinaweza kuwaumiza watu wa Ulaya kwa kiwango kikubwa sana.
Vyanzo: AFP, Reuters