1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

China yaishutumu Marekani kusambaza taharuki kuhusu Corona

Sekione Kitojo
3 Februari 2020

China imeishutumu  Marekani leo  kwa  kusambaza  hali ya  hofu  na mtafaruku  katika hatua ya  kushughulikia  virusi  hatari vya  Corona, ikiwa  ni  pamoja  na  kuweka  marufuku ya kusafiri  dhidi ya Wachina.

https://p.dw.com/p/3XC5K
China Wuhan Huoshenshan Hospital Coronavirus
Picha: picture-alliance/dpa/C. Min

Wakati huo huo  China  imekamilisha  hospitali  mpya  kwa ajili  ya  wagonjwa  wa  homa ya  virusi vya  corona mjini Muhan, wakati idadi  ya  vifo ikipanda  na  kufikia  watu 360. 

Indonesien Rückholung von Staatsbürgern aus Wuhan
Maafisa wa afya wakiwapulizia dawa wasafiri wanaowasili IndonesiaPicha: Reuters/Antara Foto

Msemaji wa  wizara  ya  mambo ya  kigeni  nchini  China  Hua Chunying  amesema  katika  mkutano  wa  kila  siku  na  waandishi habari  kuwa  Marekani  haitatoa  "msaada  wowote wa  maana" na imekuwa tu ikisambaza  hali ya  taharuki.

Marekani  siku  ya  Ijumaa  ilitangaza  dharura ya  kiafya  na marufuku  ya  muda  ya  raia  wa  kigeni  kuingia  ambao  walisafiri kwenda  China  katika  muda  wa  wiki  mbili  zilizopita, katika  hatua ya  kujaribu  kupambana  na  kusambaa  kwa virusi vya  corona. Vizuwizi  vingine  vipya  vitawekwa  pia  kwa  raia  wa Marekani, ambao  kurejea  kwao  kutoka  katika  jimbo kulikozuka  ugonjwa  huo kutasababisha  wao  kuwekwa  katika  mahali  maalum  ambapo watakaa  huko  kwa  muda  wa  siku 14 kwa  uchunguzi.

Pamoja  na  hayo China  imekamilisha   ujenzi  wa  hospitali  kwa ajili ya  wagonjwa  wa  virusi  hivyo  vya  corona. Hospitali  ya Huoshenshan, ikimaanisha  mungu  wa  moto, ilijengwa  katika  muda wa  wiki  mbili , wakati  maafisa  wakichukua  hatua  za  haraka kudhibiti  kusambaa  kwa  ugonjwa  huo unaoambukizwa  kupitia virusi  vya  corona  ambapo watu 17,000  nchini  humo wameambukizwa.

China, Wuhan: Notfall-Krankenhaus in zehn Tagen erbaut
Hospitali mpya itakayokuwa na vitanda 1,000 kwa wagonjwa wa virusi vya coronaPicha: picture-alliance/dpa

Hospitali yakamilika

Hospitali  hiyo  mpya  ambayo , itakuwa  na wauguzi  na  madaktari 1,400 na  vitanda 1,000, iko tayari  kupokea  wagonjwa leo Jumatatu, mkurugenzi mkuu  wa  hospitali  hiyo Zhang Siming amekieleza  kituo cha  utangazaji cha  taifa  CCTV.

China  pia  imesema  inahitaji  kwa  haraka  vifaa vya kitabibu  vya kujikinga. Hofu  ya  virusi imewaingia  watu  katika  nchi  hiyo  yenye idadi  kubwa  ya  watu  wanaofikia  bilioni 1.4, katika  vifaa  vya kufunika  mdomo  na  pua  ambavyo  hutumika  mara  moja  tu, wakati  waganga  wanaohusika  katika  matibabu  ya  wagonjwa  wa virusi  hivyo  katika  vituo  vya  matibabu  wameripoti  upungufu wa vifaa  hivyo.

Hongkong Streik von Krankenhauspersonal
Wauguzi na madaktari mjini Hong Kong wakiwa katika mgomo Picha: Reuters/T. Siu

"Kile  ambacho  China  inahitaji  haraka  kwa  sasa  ni  "vifuniko hivyo vya  pua  na  mdomo,nguo maalum za  kujikinga, pamoja na miwani maalum," msemaji wa  wizara ya  mambo ya  kigeni  Hua Chunying  amesema  katika  taarifa  kwa  waandishi  habari.

Wakati  huo  huo  katika  mji  wa  Hong Kong  mamia  ya wafanyakazi  wa  hospitali  wameanza  mgomo  leo  kudai  serikali ifunge  mpaka  na  China  bara  ili  kuzuwia  kusambaa  kwa  virusi vya  corona na  kupunguza  shinikizo katika  sekta  ya  fya.

nayo Urusi  inapanga  kuanza  kuwaondoa  raia  wake  kutoka  mji wa  Wuhan, kitovu cha  ugonjwa  wa  virusi  vya  corona, na imesitisha  safari  za  moja  kwa  moja  za  treni  kwenda  China.