China yaongoza kwa kuwatupa jela waandishi wa habari
11 Desemba 2019Kalamu, kitabu na vifaa vya mwanahabari haviko tena salama. Kwa mujibu wa ripoti ya kamati ya kuwalinda wanahabari iliyo na makao yake mjini New York, Marekani - CPJ, mataifa ambayo yametajwa kuwa hatari na yenye mazingira magumu ya kufanyia kazi kwa waandishi wa habari ni Uturuki, Saudia Arabia, Misri, Eritrea, Vietnam na Iran.
Wengi wa wale ambao wanahudumu vifungo gerezani wanakabaliwa na mashtaka ya kuipinga serikali ama tuhuma za kuandika habari za uongo. Kamati hiyo ya CPJ imesema kuwa imewahesabu waandishi wa habari wasiopungua 48 waliofungwa nchini China, idadi hiyo ikiwa mmoja zaidi ya mwaka 2018 wakati ambapo Rais Xi Jinping anaongeza juhudi za kudhibiti vyombo vya habari.
Takwimu hizo za CPJ zimeiweka China mbele ya Uturuki, ambayo iliwafunga waandishi wa habari 47 ikiwa ndiyo idadi kubwa kufungwa nchini humo katika muda wa miaka mitatu iliyopita, huku Saudia Arabia na Misri zikiwa katika nafasi ya tatu duniani kwa kuwafunga wanahabari 26 kila mmoja.
Nchini Saudia Arabia, hakuna mashtaka yoyote yaliyofunguliwa dhidi ya wanahabari 18 walioko kizuizini huku CPJ ikionesha wasiwasi kuhusu mateso wanayopitia wanahabari hao yakiwemo kupigwa, kuchomwa moto, na kunyimwa chakula.
Licha ya idadi ya waandishi wa habari waliofungwa nchini Uturuki kupungua kutoka 68 ya mwaka uliopita hadi 47 mwaka huu, haimaanishi kuwa hali ya utendajikazi nchini humo kwa wanahabari imeimarika, ripoti ya CPJ imesema.
Ripoji ya CPJ inaongeza kuwa juhudi za rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan zimefanikiwa kukandamiza uhuru wa vyombo vya habari hasa kuzima wanahabari wanaoandika habari za ukosoaji wa serikali.
CPJ imesema kuwa serikali ya Uturuki imefunga zaidi ya vituo 100 vya habari na kuwabandikia mashtaka ya ugaidi wafanyakazi kwenye vituo hivyo. Hatua hiyo imewakosesha kazi wanahabari wengi na imetafsiriwa kama mbinu ya kuwatisha.
Ripoti ya CPJ pia imesema utawala wa kimabavu, ukosefu wa utulivu na maandamano ambayo yamekuwa yakifanyika katika eneo la Mashariki ya kati kumesababisha ongezeko la idadi ya wanahabari waliofungwa katika eneo hilo.
Wanaharakati wanaotetea haki za wanahabari wanahoji kuwa idadi ya wanahabari 250 waliofungwa bado iko juu na yenye kutia hofu japokuwa idadi hiyo iko chini tofauti na wanahabari 255 waliofungwa mwaka 2018 na 273 mwaka 2016.