Idadi ya maambukizi ya virusi vya Corona yaongezeka
10 Februari 2020Idadi ya waliofariki kutokana na virusi vya corona nchini China bara imefikia watu 908, baada ya vifo vipya 97 kuripotiwa katika muda wa saa 24 hapo jana usiku. Wakati huo huo nchi hiyo imesajirli visa vipya 3,062 vya ugonjwa huo.
Hiyo ni nyongeza ya asilimia 15 kutoka siku ya Jumamosi ambayo imegeuza mwelekeo ambapo kila siku maambukizi mapya yamekuwa yakipungua. Hapo jana, msemaji wa serikali alisema kuwa idadi ya visa vya maambukizi iliyopungua ilionyesha kuwa mikakati ya kuzuia kuenea kwa virusi hivyo imefanikiwa.
Nahodha wa meli ya anasa iliyowekwa chini ya karantini mjini Yokohama karibu na mji mkuu wa Japan, Tokyo, amesema kuwa visa 66 vipya vya maambukizi ya homa ya corona viligunduliwa katika meli hiyo. Hili ni ongezeko katika visa 70 vilivyokuwa vimeripotiwa awali.Waziri wa afya wa Japan Katsunobu Kato, amesema kuwa serikali ya Japan inafikiria kuwafanyia uchunguzi abiria wote 3,771 na wafanyikazi wa meli hiyo ya Diamond Princess ambapo watu hao watalazimika kusalia katika meli hiyo hadi majibu ya uchunguzi huo yatakapotolewa.
Maafisa wa afya wanajitahidi kupeleka dawa zinazohitajiwa na abiria zaidi ya 600. Kato amesema kuwa wanajitahidi kadri ya uwezo wao kuhakikisha kuwa kila mmoja anasalia kuwa na afya njema. Zaidi ya visa 360 vimethibitishwa nje ya China bara ikiwa ni pamoja na vifo viwili katika jimbo la Hong Kong ambalo pia limethibitisha visa 36, pamoja na Ufilipino.
Wakati huo huo, serikali ya Uingereza hii leo imeonya kuwa mripuko huo wa virusi vya Corona ni hatari kwa umma na kutangaza mikakati mipya ya kuwalinda raia wake. Taarifa kutoka kwa wizara ya afya imesema kuwa kuenea kwa virusi hivyo kunahusisha tishio kubwa kwa afya ya umma.
Idadi ya watu waliofariki kutokana na virusi hivyo vipya vya Corona, imepita ile ya watu 774 wanaoaminika kufariki katika janga la mwaka 2002-03 la matatizo ya kupumua ambalo lilitokana na mripuko mwingine wa virusi vya SARS nchini China. Idadi ya walioambukizwa pia ni kubwa kufikia visa 40,171 katika eneo la China bara ikilinganishwa na idadi ya visa 8,098 ya maambukizi ya virusi vya SARS.
China imejenga hospitali mbili mpya na kuwapeleka madaktari wa ziada, wauguzi na wahudumu wengine wa afya mjini Wuhan, mji ulio na idadi ya watu milioni 11 katika eneo la Kati kati mwa China ambalo ni kitovu cha mripuko wa virusi hivyo vya Corona.Njia nyingi za kuingia mjini humo zimefungwa tangu Januari 23 huku hatua hiyo ikiendelezwa katika miji mingine iliyo na jumla ya watu zaidi ya milioni 60.