China yasimamisha ushirikiano wa kisheria na nchi kadhaa
28 Julai 2020China imetangaza jumanne kuwa inasimamisha mkataba wa kubadilisha wahalifu kati ya kisiwa chake cha Hong Kong na mataifa ya Canada, Australia na Uingereza, kama ulipizaji kisasi kwa maamuzi ya nchi hizo baada ya kupitishwa kwa sheria ya China ya usalama wa taifa iliyoleta utata.
Canada, Australia na Uingereza ni wanachama wa muungano wa kiintelijensia ujulikanao kama ''Five Eyes'' yaani macho matano, ambao unazijumuisha pia Marekani na New Zealand. Tayari New Zealand imekwishasimamisha mkataba wa kubadilishana wahalifu kati yake na Hong, na Marekani imeashiria kuwa inajiandaa kuchukua hatua kama hiyo.
Akitangaza uamuzi wa nchi yake, msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya China Wang Wenbin amesema Uingereza, Canada na Australia zimeingiza siasa katika ushirikiano wa kisheria na Hong Kong,hali ambayo amesema imeathiri pakubwa ushirikiano huo.
''China imeamua kusitisha mikataba ya kubadilisha wahalifu na vilevile uhusiano wa kisheria baina ya HongKong na Canada,Australia na Uingereza'',alisema Wang.
Uingereza ilichukuwa hatua hiyo wiki iliopita ikifuatia Australia na Canada.Uingereza ilielezea kwamba sheria ya usalama ya China huko HongKong imebadili dhana muhimu ya mikataba hiyo.