1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

China yatetea mradi wake wa miundombinu

25 Aprili 2019

Rais wa China Xi Jinping na Waziri Mkuu Li Keqiang wamekutana na viongozi wa mataifa kutoka Kenya, Ufilipino, Mongolia, Mnyamar na Hungary, siku moja kabla ya mkutano wa pili wa Mradi wa Miundombinu mjini Beijing.

https://p.dw.com/p/3HRg6
Präsident der Volksrepublik China Xi Jinping anlässlich der Eröffnung des "Panda Garden" im Berliner Zoo
Picha: picture-alliance

Xi kwanza alikutana na Rais wa Ufilipino Rodrigo Duterte na kisha Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya kwa ajili ya mazungumzo yanayohusu mahusiano ya nchi zao.

Awali wakati wa ufunguzi rasmi wa mkutano huo, China iliutetea vikali mradi wake huo wa Miundombinu wakati ikiufungua rasmi mkutano huo wa kilele kwa kutoa ahadi ya kuondoa hofu kuhusu madeni yanayohusishwa na sera yake hiyo kuu ya kigeni. Mradi huo wa kipaumbele kwa Rais Xi Jinping ni wazo la kuufufua upya mtandao wa jadi wa kibiashara ulioyaunganisha mabara ya Asia, Ulaya na Afrika kupitia uwekezaji mkubwa wa miradi ya baharini, barabara na reli.

Mradi huo unalenga kujenga miundombinu ya kisasa inayohitajika kwa kiasi kikubwa katika mataifa yanayoendelea, lakini Marekani inauita "mradi batili" na wakosoaji wanaonya kuwa ni "mtego wa madeni" unaozifaidi kampuni za China. Waziri wa Fedha wa China Liu Kun amesema China itazindua mfumo wa "kuepusha kitisho cha madeni".

Rais Jinping pamoja na waziri wake mkuu Le Keqiang wamekutana hii leo na marais wa Ufilipino, Kenya, Myanmar, Mongolia na Hungary. Rais Jinping alianza kwa kukutana na rais Rodrigo Duterte wa Ifilipino na baadaye Uhuru Kenyatta wa Kenya kwa mazungumzo ya faragha kabla ya kukutana na rais wa Mongolia. 

Kenia Uhuru Kenyatta
Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya alipata wasaa wa kuzungumza na rais Xi Jinping wa China kuhusu mashirikiano baina yaoPicha: imago/i Images

Kwa upande wake waziri mkuu Keqiang alikutana na kiongozi wa Myanmar Aung San Suu Kyi kwa mazungumzo na kushuhudia kusainiwa kwa makubaliano kadhaa kuhusiana na mradi huo, lakini pia mashirikiano, na baadae kutiliana saini makubaliano ya ushirikiano wa kiuchumi na waziri mkuu wa Hungary Viktor Orban.

IMF wakaribisha hatua hiyo ya China, Marekani yapeleka washiriki wa ngazi za chini kwenye mkutano huo.

Mjumbe wa ofisi ya chama cha Kikomunisti Huang Kunming kwenye ufunguzi wa mkutano huo wa kilele wa siku tatu amesema wanataraji kutumia kusanyiko hilo kuondoa hali ya kutokuelewana na minong'ono kuhusu mradi huo wa BRI. Wanaharakati wa mazingira kwa mfano wameituhumu China kwa kufadhili robo ya vinu vipya vya nishati vinavyotumia makaa ya mawe kote duniani wakitaka kuchukuliwa hatua za kuheshimu malengo ya kulinda mazingira.

Mkuu wa shirika la fedha la kimataifa, IMF Christine Lagarde amesema wanalikaribisha tangazo hilo la Liu na kuendelea kuangazia mafanikio ya muda mrefu ya mradi huo wa BRI, na kusema ni hatua nzuri na zinazoelekea katika mkondo sahihi.

Waziri wa uchumi wa Ujerumani Peter Altmaier amesafiri hii leo kwenda Beijing. Atakuwa miongoni mwa wawakilishi 100 kwa ajili ya mkutano huo utakaofunguliwa rasmi na rais Xi Jinping na unaofanyika miaka mitano baada ya China kuzindua mkakati huo kwa mara ya kwanza, kwa lengo la kuiunganisha na Ulaya, Afrika na Amerika ya Kusini.

Jumla ya wawakilishi kutoka nchi 37 wanahudhuria mkutano huo. Marekani pekee ndio imetuma wawakilishi wa ngazi ya chini hatua inayoashiria kutokukubaliana kwake na mradi huo. Awali iliupinga uamuzi wa Italia wa kusaini makubaliano ya mradi huo, ikiwa ni taifa la kwanza miongoni mwa mataifa yaliyoinukia kiuchumi, G7.