China yatumia lugha kali kuionya Taiwan kuhusu uhuru
29 Januari 2021China imetumia lugha kali dhidi ya Taiwan, ikionya kuwa shughuli za kijeshi na ombi la kutaka uhuru kwa kisiwa hicho vinamaanisha vita. China imesema jeshi lake litajibu kwa uchokozi na uingiliaji kutoka nje.
Taiwan, inayodaiwa na China kama ardhi yake, imesema mwishoni mwa wiki iliyopita China ilituma ndege zake za kivita kwenye anga yake ya kusini magharibi, hali iliyosababisha Marekani kuionya China kusitisha shinikizo dhidi ya Taiwan.
China, ambayo inaona kuwa kisiwa hicho ni sehemu yake muhimu, inashuku utawala wa Taiwan kwamba unataka kutangaza uhuru huo, wakati Rais Tsai Ing-wen anaona kuwa hatua hii sio lazima kwa vile anaona kuwa tayari imefikiwa.
Wu Qian, msemaji wa wizara ya ulinzi ya China amesema Taiwan ni sehemu isiyogawika ya China.
"Shughuli za kijeshi zinazofanywa na jeshi la Ukombozi la Watu wa China katika Mlango wa Taiwan ni muhimu kushughulikia hali ya sasa na kulinda uhuru wa kitaifa na usalama. Hili ni jibu zito kwa mataifa ya nje yanayotaka kuingilia masuala ya ndani ya China na makundi yanayotetea 'Uhuru wa Taiwan'. Wale wanaocheza na moto watajichoma wenyewe na 'Uhuru wa Taiwan' unamaanisha vita."
Marekani yasema Taiwan inahaki kujihami
Licha ya kwamba China haijasitisha nia ya kutumia nguvu ili Taiwan iendelee kubaki chini ya udhibiti wake, lakini sio kawaida ya Beijing kutoa vitisho vya aina hiyo.
Alipohojiwa kuhusu matamshi ya China, msemaji wa wizara ya ulinzi ya Marekani, John Kirby alisema kuwa hakuna sababu yoyote ya kupelekea vita kufuata mzozo wa hivi sasa baina ya China na Taiwan. Alielezea pia uungwaji mkono wa kijeshi wa muda mrefu wa Marekani kwa ajili ya kujihami kwa Taiwan.
Kuongezeka kwa operesheni za kijeshi za China kunaendana na kuwasili kwa meli kubwa ya Marekani na kikosi cha majini katika Bahari ya Kusini ya China.
Baraza linalohusika na masuala ya China huko Taiwan limesema China inatakiwa kufikiria vyema na kutopuuzia nia ya kisiwa cha Taiwan ya kuhifadhi uhuru na demokrasia yake.
China kutozitambua pasi za Wahong Kong
Huku hayo yakijiri, China imesema haitozitambua tena pasi za kusafiria zinazotolewa na Uingereza kwa baadhi ya raia wa HongKong. Hiyo ni baada ya Uingereza kuongeza hati za raia hao kuishi kwenye ardhi yake.
Serikali ya Uingereza ilitangaza kuanza kutekeleza hatua hiyo Jumapili ijayo Januari 31 kwa watu wanaoshikilia pasi hizo za kusafiria. Ikiwa ni jibu kwa hatua ya China ya kupitisha sheria mpya ya usalama huko Hong Kong.