Chissano ahimiza juu ya suluhisho Sahara Magharibi
27 Aprili 2016Mjumbe huyo maalum wa Umoja wa Afrika kuhusu Sahara Magharibi , Rais wa zamani wa Msumbiji Joachim Chissano ambaye kuteuliwa kwake mwaka 2014 kulipingwa na Morocco, aliuambia mkutano usio rasmi wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwamba shughuli za ujumbe wa Umoja huo zinapaswa kuachwa ziendelee kikamilifu na kwamba umma wa Sahara Magharibi lazima upewe nafasi ya kuchaguwa wenyewe mustakbali wao kwa njia huru. Chissano alisisitiza kwamba hiyo ndiyo njia pekee ya kupata suluhisho.
Alisema tatizo la Sahara Magharibi linaweza likaonekana kuwa ni dogo, lakini kuripuka kwake, kunaweza kukasabisha kile alichokiita kuwa sawa na msitu unaowaka moto na kwamba hilo halinabudi kuepukwa. Moroccpo iliitwaa kwa nguvu Sahara Magharibi, koloni la zamani la Uhispania 1975 na kupigana na Chama cha Ukombozi wa eneo hilo POLISARIO.
Usimamishaji mapigano ulifikiwa 1991 kutokana na juhudi za Umoja wa Mataifa na Umoja huo kutuma kikosi cha kusimamia amani kinachojulikana kama MINURSO ukiwa pia na lengo la kuandaa kura ya maoni kuhusu mustakbali wa eneo hilo, jambo ambalo hadi sasa limeshindwa kufanyika.Morocco inashikilia kwamba Sahara Magharibi yenye utajiri mkubwa wa madini kuwa jimbo lake la Kusini na imependekeza ipewe madaraka makubwa ya utawala wa ndani, lakini Chama cha POLISARIO kinashikilia kwamba Sahara Magharibi klazima ijitawale wenyewe kwa umma kupewa fursa ya kujiamulia hatima yao kwa njia ya kura ya maoni, kama ilivyofafanuliwa katika maazimio ya Umoja wa Mataifa.
Morocco ilifukuza watumishi wa Kiraia wa Umoja wa Mataifa
Mnamo mwezi uliopita Morocco iliwafukuza watumishi wa kiraia wa Umoja wa Mataifa baada ya Katibu mkuu wa Umoja huo Ban Ki-moon kutumia neno, "Uvamizi," alipokuwa akizungumzia Sahara Magharibi kufuatia ziara yake katika kambi moja ya wakimbizi wambao wamekuwa wakiishi Algeria kwa zaidi ya miaka 40 .
Umoja wa Mataifa unasema kukimbia kwao kumesababisha ujumbe wake ushindwe kutekeleza jukumu lake . Ban Ki-moon , Joachim Chissano na wanasiasa watu wengine wengi maarufu, wameonya kwamba hatua ya Morocco kuwafukuza watumioshi wa Umoja huo lazima ibatilishwe kwa sababu inaweza kugeuka mfano mbaya wa kuigwa na nchi nyengine.
Katibu mkuu wa POLISARIO na Rais wa Sahara Magharibi inayotambuliwa kuwa dola huru na theluthi mbili ya wanachama wa Umoja wa Afrika, Mohammad Abdulaziz ameonya kwamba pindi Morocco haitashinikizwa kuwarejresha watumishi wa Umoja wa Mataifa, itakuwa imepewa kibali kwa kufanya uchokozi kwa hatua za kijeshi. Abulaziz akisema pindi hilo litatokea watu wa Sahara Magharibi watajibu kwa njia zote halili , ikiwa ni pamoja na mapambano ya mtutu wa bunduki.
Chissano amesisitiza Morocco ni sehemu ya Afrika, ingawa si mwanachama wa Umoja wa Afrika na kwamba Afrika ina jukumu la kisiasa na uadilifu kutafuta suluhisho la matatizo yanayoölikabili bara hilo na hivyo haunabudi kuchukua nafasi ya usoni kutafuta suluhisho la mzozo wa Sahara Magharibi. Kikao cha jana cha Baraza la Usalama kilifanyika siku chache kabla ya Aprili 30 , tarehe ya kumalizika muda wa ujumbe wa Umoja Mataifa kuhusu Sahara Magharibi, katika wakati ambao wanachama wake wanalumbana kujaribu kukubaliana juu ya azimio la kurefusha ujumbe huo.
Kikao hicho kilifanyika katika ukumbi wa mkutano wa Umoja wa Mataifa na sio kwenye Baraza la usalama, kwasababu Ufaransa , mshirika wa karibu wa Morocco, ilipinga maelezo ya mjumbe maalum wa Umoja wa Afrika yasiwe rasmi. Ufaransa pia imekuwa ikizuwia hatua za kuitishwa kura ya maoni na ukaguzi wa haki za binaadamu katika Sahara Magharibi.
Mwandishi: Mohammed Abdul-Rahman, AP
Mhariri:Yusuf Saumu