Clinton ataka Assad abanwe zaidi
20 Aprili 2012Matamshi ya Clinton yamekuja wakati ambapo katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon anamlaumu rais Bashar Assad kwa kushindwa kuheshimu mpango wa amani ulioanza kutekelezwa wiki iliyopita.
"Tunahitaji kunendeleza kazi na kuelekeza nguvu zetu kwenye kupata ruhusa ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ili tupate mamlaka ya kusonga mbele muda utakapowadia," alisema Clinton
Hotuba ya Clinton ilijikita katika pendekezo la Marekani la kulitaka kundi la marafiki wa Syria kuandaa mkakati wa dharura endapo mpango wa amani wa Umoja wa Mataifa na Jumuiya ya Nchi za Kiarabu ulioandaliwa na mjumbe maalumu Koffi Annan utashindwa kufikia lengo.
Ingawa Marekani inatambua kwamba uwezekano wa kumuondoa Assad kwa sasa ni mdogo, azimio la Umoja wa Mataifa analolitaka Clinton linaweza kuwaongezea nguvu waasi wanaopambana na serikali yake.
Alisema kinachotakiwa kwa sasa ni kuongeza shinikizo kwa baraza la Usalama ili kuandaa rasimu ya azimio la vikwazo zaidi ikiwa ni pamoja na vya usafiri, fedha, silaha vitakavyolaazimisha utawala wa Assad kutekeleza hatua sita za mpango wa Annan.
Hofu ya kura ya turufu
Lakini jaribio lolote la vikwazo vya Umoja wa Mataifa litakumbana na upinzani kutoka kwa washirika wa Syria, Urusi na China ambazo zina kura za turufu katika Baraza la usalama. Tayari Urusi na China zimepiga turufu dhidi ya maazimio mawili ya Umoja wa Mataifa kulaani utawala wa Assad.
Clinton alisema amezungumza na waziri wa mambo ya Nje wa Urusi, Sergio Lavrov na kumueleza kuwa hali iliyoko nchini Syria inazidi kudorora.
Naye waziri wa mambo ya nje wa Uingereza William Hague alisema: "Kama hatua ya kusitisha mapigano haileti ufanisi na mpango wa Annan haufuati, basi ni wazi kwamba anayehusika ni serikali ya Syria na ndiyo maana tunaipia urusi jukumu la kuishinikiza serikali hiyo kutekeleza."
Msimamo wa Urusi
Lakini Waziri wa mambo ya nje wa Urusi Sergio Levrov amesema pamoja na kuwepo ukiukaji mdogo, lakini hatua ya kusitisha mapigano ilikuwa na ufanisi na kuongeza kuwa jukumu la kulinda haki za binadamu, usalama na uhuru wa nchi viko mikononi mwa Syria wenyewe.
Mnamo wiki za hivi karibuni, Urusi imekuwa ikimkosoa mshirika wake Assad kutokana na hali inayozidi kuwa mbaya nchini humo, lakini wakati huo huo imeyakosoa pia mataifa ya kigeni kwa kuwaunga mkono wpinzani nchini Syria.
Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga\APE\AFPE
Mhariri:Mohammed Abdul Rahman