Colin Powell afariki dunia
18 Oktoba 2021Mwana huyu wa kiume wa wahamiaji kutoka Jamaica ameaga dunia kwa ugonjwa ambao tayari umeshachukuwa maisha ya mamilioni ya watu ulimwenguni, licha ya yeye kuwa alishachoma chanjo dhidi ya virusi vya korona.
Colin Powell alikuwa mmoja kati ya Wamarekani weusi wenye nguvu sana kwa miongo kadhaa. Marais watatu wa Republican walimteuwa kushika nyadhifa za juu, na akafikia ngazi ya juu jeshini wakati Marekani ikijijenga upya baada ya aibu iliyoipata kwenye Vita vya Vietnam.
Powell, ambaye alijeruhiwa kwenye vita hivyo, alihudumu kama mshauri wa masuala ya usalama wa Rais Ronald Reagan kutoka mwaka 1987 hadi 1989. Wakati wa Vita vya Ghuba vya mwaka 1991, ambapo majeshi ya Marekani yaliyoongoza vikosi vya washirika kuyatowa majeshi ya Iraq nchini Kuwait, yeye alikuwa ndiye mkuu wa majeshi chini ya Rais George Bush Mkubwa.
"Kwa heshima na taadhima, nawasilisha jina la Colin L. Powell mbele ya Baraza la Seneti la Marekani kuwa waziri wa nje wa Marekani." Alisema Rais George Bush Mdogo wakati wa kumteuwa Powell kuwa waziri wake wa mambo ya kigeni.
Siasa za wastani na utata wa Vita vya Iraq
Jenerali huyo wa nyota nne na mwanachama wa Republican mwenye msimamo wa wastani alijaribu kutaka kuwa rais wa kwanza mweusi nchini Marekani mwaka 1996, lakini mke wake, Alma, alimshawishi kubadilisha uamuzi huo kwa kukhofia usalama wake. Mwaka 2008, akakhitalifiana na msimamo wa chama chake na akamuunga mkono mgombea urais kupitia chama cha Democrat, Barack Obama, ambaye ndiye aliyekuja kuwa Mmarekani wa kwanza mweusi kuchaguliwa kuwa rais.
Licha ya mafanikio hayo, Powell daima atasalia kuhusishwa na hotuba yake yenye utata aliyoitowa tarehe 5 Februari 2003 kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, akijenga hoja ya uamuzi wa Rais George Bush Mdogo kwamba rais wa wakati huo wa Iraq, Saddam Hussein, alikuwa ni tishio kubwa kwa Marekani na ulimwengu kwani alimiliki maghala ya silaha za kemikali na kibaiolojia na hivyo lazima atiwe adabu.
Baadaye alikuja kukiri kwamba hotuba hiyo iliwasilisha mambo mengi yaliyopindishwa na alibeba dhamana ya makosa hayo. Mwaka 2005, alikiambia kituo cha habari cha ABC kwamba kosa hilo lingelisalia daima kwenye rikodi yake. Kwamba lilimuuma wakati huo na liliendelea kumuuma muda wote.