COLOGNE: Jamii na mazingira yapaswa kuheshimiwa
9 Juni 2007Kansela wa Ujerumani,Angela Merkel hii leo alipozungumza kwenye mkutano wa Kanisa la Kiprotestanti mjini Cologne alisema,lazima viwepo viwango vya kijamii na kuhusu mazingira kote ulimwenguni kwa ulinzi wa raia na vile vile vipimo hivyo lazima vitekelezwe.Kwa maoni yake utandawazi utaweza kufanikiwa kwa njia hiyo tu.Akaongezea kuwa,vipimo hivyo haviwezi kuendelea kushushwa mtu apendavyo.Kansela Merkel kwenye mkutano huo wa Kanisa la Kiprotestanti alizungumza pia na mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel kutoka Bangladesh,Muhammad Yunus. Mwanauchumi Yunus alisema,watu ni viumbe na si “ mashine za kutengenezea pesa“.
Hapo awali Merkel alisema,maafikiano muhimu yalipatikana katika mkutano wa viongozi wa G-8 uliomalizika siku ya Ijumaa mjini Heiligendamm, kaskazini ya Ujerumani.Viongozi hao walikubaliana kuchukua hatua za kupambana na ongezeko la ujoto duniani kwa kupunguza uzalishaji wa gesi zinazochafua mazingira.Vile vile wameahidi msaada wa Euro bilioni 44 kupiga vita UKIMWI,malaria na kifua kikuu barani Afrika na kutekeleza ahadi za hapo awali,kutoa pesa zaidi kwa misaada ya maendeleo.