1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

COLOGNE : Polisi yazima njama ya kushambulia shule

19 Novemba 2007
https://p.dw.com/p/CIln

Polisi katika mji wa Cologne nchini Ujerumani imesema imezuwiya njama ya vijana wawili kushambulia shule yao.

Mtuhumiwa mkuu amejiuwa hapo Ijumaa kwa kujirusha chini ya treni baada ya kuitwa katika ofisi ya mwalimu mkuu wa shule na baadae kutakiwa arudi nyumbani.Mtuhumiwa mwengine mwenye umri wa miaka 18 amekamatwa na polisi na amekiri juu ya njama hiyo.

Polisi inasema kwamba wana ushahidi kuwa vijana hao walikuwa wamepanga kuishambulia shule yao ya Georg Buechner Gymnasium kwa silaha yumkini yakiwemo mabomu ya petroli na ya mabomba.

Norbert Wagner Mkuu wa Idara ya Uhalifu anasema pia wana orodha ya majina ya walimu na wanafunzi ambao yumkini wangeliweza kuwa wahanga wa kitendo cha vijana hao wawili.

Wanafunzi wenzao darasani waliwagutusha walimu baada ya kuwaona watuhumiwa wakichunguza picha ya mauaji ya mwaka 1999 ya shule ya sekondari ya jimbo la Colorado nchini Marekani ambapo wanafunzi wawili waliwauwa wenzao 12 na baadae kujiuwa wenyewe.