1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

COP27: Viongozi kuzungumzia ongezeko la joto duniani

8 Novemba 2022

Viongozi wa ulimwengu wanatarajia kuwasilisha mapendekezo kuhusu hatua madhubuti za kuchukuliwa katika kukabiliana na ongezeko la joto duniani, wakati ambapo mkutano wa kimataifa kuhusu mazingira ukiendelea Misri.

https://p.dw.com/p/4JC2A
UN-Weltklimakonferenz COP27 - Antonio Guterres, Generalsekretär der Vereinten Nationen
Picha: picture alliance/dpa

Akizungumza Jumatatu katika mkutano huo wa Umoja wa Mataifa kuhusu mabadiliko ya tabianchi, COP27, unaofanyika katika mji wa mapumziko wa Sharm el-Sheikh nchini Misri, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ameonya kuwa ubinadamu uko katika hatari ya kuangamia na amezitaka nchi kushirikiana au kuangamia.

''Mapambano ya hali ya hewa duniani yatafanikiwa au yatashindikana katika muongo huu muhimu tulionao. Jambo moja la uhakika, wale wanaokata tamaa wana uhakika wa kushindwa. Hivyo tupambane pamoja na tushinde,'' alisisitiza Guterres.

Yawepo makubaliano kati ya nchi tajiri na maskini

Guterres ametoa wito wa kuwepo makubaliano kati ya mataifa tajiri na yale maskini duniani ili kuharakisha mageuzi ya kuachana na matumizi ya nishati ya mafuta na makaa ya mawe na kuanza kutumia vyanzo vya nishati mbadala. Amesema nchi mbili zenye uchumi mkubwa duniani, Marekani na China zina jukumu maalum la kuunganisha juhudi za kuhakikisha makubaliano hayo yanakuwa ya kweli.

Aidha, Guterres na viongozi wengine kama vile Waziri Mkuu wa Barbados, Mia Mottley wamesema ni muda muafaka kwa kampuni za mafuta kuchangia katika mfuko wa kuzisaidia kifedha nchi zinazokumbwa na athari za mabadiliko ya tabianchi.

BdTD COP27 Ludwigshafen Schornsteine auf BASF-Chemiewerk
Moshi ukitoka katika kiwanda cha kemikali cha BASF kilichoko Ludwigshafen, Ujerumani,Picha: Michael Probst/AP/picture alliance

Wazo la kuzitoza kodi kubwa kampuni za mafuta na gesi lilipata msukumo mkubwa katika miezi ya hivi karibuni, ambapo kampuni hizo zimepata faida kubwa kutokana na kuongezeka sana kwa bei ya nishati, huku watumiaji wakihangaika kuleta joto kwenye nyumba zao na kujaza mafuta kwenye magari.

Waziri Mkuu wa Antigua na Barbuda, Gaston Browne, amesema viwanda vya mafuta na gesi vinaendelea kujipatia faida ya takribani dola bilioni tatu kila siku, na hivyo ni muda muafaka kwa kampuni hizo kulazimika kulipa ushuru wa kimataifa wa gesi ya kaboni kutokana na faida hizo, kutokana na hasara na uharibifu wanaosababisha.

Sall: Maslahi ya Afrika yasipuuzwe

Rais wa Senegal, Macky Sall amesema ni vyema kuwa ni wazi wanaunga mkono kupunguzwa kwa utoaji wa gesi chafu ya kaboni, lakini Waafrika hawawezi kukubali maslahi yao muhimu yapuuzwe.

Wakati huo huo, ripoti inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa imeeleza kuwa nchi zinazoendelea na zile zinazoinukia ukiitoa China, zinahitaji uwekezaji wa zaidi ya dola trilioni mbili kwa mwaka ifikapo mwaka 2030, iwapo ulimwengu unataka kuzuia ongezeko la joto duniani na kukabiliana na athari zake.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo ambayo imetolewa Jumanne nchi tajiri zinapaswa kutambua kwamba ni kwa maslahi yao binafsi pamoja na pia suala la haki kutokana na athari zinazosababishwa na viwango vyao vya juu vya uzalishaji wa sasa na wa zamani, kuwekeza katika hatua za hali ya hewa kwenye soko linaloinukia na nchi zinaoendelea.

(AP, AFP, Reuters)