CORONA : Nchi za Ulaya zalegeza vizuwizi vyao
11 Mei 2020Viongozi wamechukuwa hatua hiyo kwa hali ya tahadhari kubwa kufuatia wasiwasi wa kuweko na wimbi jipya la maambukizi.
Idadi ya visa vya maambukizi ya virusi vya Corona nchini Ujerumani inaongezeka. Ufaransa na Uhispania zimelegeza vikwazo vya karantini kwenye miji mikubwa na huko Marekani makamu wa rais Mike Pence ameatarajiwa kurudi kazini Jumatatu baada ya msaidizi wake kuambukizwa na Corona.
India iliripoti Jumatatu idadi kubwa kabisa ya maambukizi ya virusi vya Corona kuwahi kutokea nchini humo kwa siku ambavyo ni visa 4,213 kwenye taifa hilo lenye wakaazi bilioni 1.3 ambako tayari zaidi ya visa 67,000 vikiwemo vifo 2,602 kuripotiwa.
Licha ya ongezeko la visa hivyo, India ilianzisha pia mchakato wa kulegeza vikwazo vya kutotoka nje na kuanzisha usafiri wa treni ambao wakati wa kawaida husafirisha watu milioni 23 kwa siku. Amri ya kutotoka nje inatarajiwa kumalizika Mei 17.
Nchini China, eneo la starehe la Shanghai Disneyland, lilifungua milango yake katika dalili za kurejesha hali ya kawaida kwenye nchi hiyo ambayo ndio chanzo cha ugonjwa huu wa Corona. Jumatatu,China iliripoti visa vipya 17 vya Corona, vitano kutoka mji wa Wuhan. Ongezeko hilo la visa ambalo limekuja baada ya wiki ya kuripoti visa chini ya kumi vimeongeza wasiwasi kwa wamaafisa wa afya.
Korea Kusini iliarihisha kufungua shule baada ya kuripotiwa kwa visa kadhaa kutokana na watu waliohudhuria kilabu cha usiku. Shule kwa ajili ya wanafunzi wa sekondari zimetarajiwa kufunguliwa Jumatano.
Nchini Sri Lanka serikali iliwataka wafanya kazi wa sekta ya umma na wale wa sekta binafsi kurejea kazini baada ya wiki nane za kutotoka nje. Lakini mikahawa na maduka ya nguo na maeneo ya mazoezi yatabaki yakufungwa. Usafiri wa umma utatumiwa tu na watu wanaokwenda kazini. Sri Lanka imeripoti visa 856 na vifo 9 pekee.
Kwa upande wake Bangladesh imeripoti leo idadi yake kubwa kabisa ya maambukizi ya virusi vya Corona, ikiwa ni watu 1,034 na kufikia idadi jumla ya watu 15,691 walioambukizwa na vifo 239.
Nchini Ujerumani, serikali inapanga kuwekeza kwenye shirika la kitaifa la reli, Deutsche Bahn, baada ya shirika hilo kuelezea kwamba lina matatizo makubwa ya kifedha kutokana na janga hili la Corona. Likitaja nyaraka za siri za waziri wa fedha wa Ujerumani, shirika la habari la DPA, linaelezea kwamba, Deutshe Bahn imepoteza euro bilioni 13.5 kutokana na janga hili la Corona. Serikali inataka kuwekeza asilimia 80 ya fedha hizo katika kuongeza kiwango chake cha hisa kwenye shirika hilo. Hatua hiyo inatakiwa kuidhinishwa na shirika la mikopo la umoja wa Ulaya.
Waziri wa uchumi wa Ujerumani, Peter Altmaier alisema kwamba ugonjwa huu wa Coroa hauwezi kuzuwiya ujenzi wa kiwanda cha Tesla kwenye jimbo la Brandenburg. Kampuni ya Tesla imepanga kutengeneza kila mwaka hapa nchini Ujerumani magari 5,000 yanayoendeshwa kwa nishati ya umeme.
Huko nchini Senegal, mji wa Touba ambao ulikuwa ndio kitovu cha ugonjwa wa Corona umekumbana na wimbi la pili la maambukizi. Amri ya kutotoka nje ya wiki mbili ilichukuliwa machi 26 wakati visa 27 viliporipotiwa kwenye mji huo.Toka hapo tayari ni visa 190 ambavyo vimeripotiwa.
Kwa jumla Senegal iliripoti visa 1,700 na vifo 19. Hiyo ni idadi ndogo ukilinganisha na nchi nyingi barani Ulaya. Lakini shirika la afya ulimwenguni lilitahadharisha kwamba huenda Afrika ikawa ndio kitovu kingine cha ugonjwa huo.