Corona yatishia uhuru wa habari
21 Aprili 2020Katika tathmini yake ya mwaka kuhusu uhuru wa habari duniani, shirika hilo limeonya kuwa kadhia ya kiafya katika ulimwengu katika kipindi hiki inatumika kama kigezo kwa serikali kutumia fursa ya ukweli kwamba siasa zimewekwa kando, ili kufanikisha hatua ambazo hazingewezakana kufanyika katika nyakati za kawaida. Korea Kaskazini imeorodheshwa katika nafasi ya mwisho ya faharasa ya viwango vya uhuru duniani. Kama ilivyokuwa mwaka wa 2019, Norway imeongoza tena orodha hiyo ya nchi 180.
Kwa ujumla ripoti inaeleza uhuru wa habari kwa Marekani umekuwa wa kuridhisha, lakini pia imesema vitisho na vitendo vya kuwashurutisha waandishi vimeendelea kuwa tatizo kwa kipindi cha mwaka uliopita. Katika orodha ya hali ya uhuru wa habari Marekani imewekwa katika nafasi ya 45, ikiwa nyuma ya mataifa kama ya Ulaya, Afrika, Asia, Amerika ya Kusini na Caribbean.
Rais Trump atajwa kichocheo cha ubinywaji wa habari
Ripoti hii ya shirika la waandishi wa habari wasio na mipaka inamtaja rais wa Marekani Donald Trump kama mtu mwenye uhasama kwa baadhi ya waandishi wa habari na vyombo vya habari na mara kadhaa amesikika akitoa tuhuma za habari za uongo kwa neno la "fake news" kwa vyombo husika. Shirika hilo limesema hali ya kuongezeka kwa chuki dhidi ya waandishi na vyombo vya habari nchini Marekani imesababisha hali kama hiyo ya chuki kwa sekta ya habari kutekelezwa na viongozi wengine mbalimbali katika maeneo ya ulimwengu.
Vitendo hivyo vimeendelea kuwa vibaya zaidi katika kipindi hiki cha maambukizi ya virusi vya corona na utawala wa Trump umetajwa kufanya ukandamizaji wa habari katika taarifa zake kuhusu janga hilo kila uchao. Lakini kwa upande mwingine kuna kitisho cha suala la uchumi kwa waandishi katika siku za usoni. Hilo linahusisha uhaba wa kazi, na udhaifu wa kanuni za usimamizi wa teknolojia ya kidijitali ambao umezusha vurugu katika mchakato wa utoaji taarifa. Jambo hilo linajitanabaisha katika ugumu wa kutofautisha kati ya ukweli, uongo, propaganda na matangazo.
Shirika hilo lenye kufuatilia muenendo wa waandishi wa habari limesema changamoto kubwa ambayo sekta ya habari inakabiliana nayo ni kasi ya kuenea kwa taarifa za uongo ambazo wakati mwingine zinasambaa kwa kasi kama ilivyo kwa virusi vya corona. Kutokana na yote ambayo yameanishwa katika ripoti hiyo shirika hilo limewataka wadau katika pande tofauti wenye kuitakia mema sekta ya habari kufanya kampeni za kuhimiza waandishi wa habari kutimiza wajibu wao kwa maslahi ya umma.
Mwandishi: Sudi Mnette APE
Mhariri:Josephat Charo