Covid-19: Ujerumani haina mpango wa kufunga mipaka
11 Machi 2020Ujerumani imerikodi visa karibu 1, 300 kufikia leo, lakini mpaka sasa ni watu watatu tu waliofariki - kiwango cha chini ambacho watalaamu wamesema kimetokana na upimaji wa haraka baada ya kuzuka kwa mripuko huo.
Merekel amesema kwenye mkutano uliotishwa haraka wa waandishi habari mjini Berlin, kwamba ni muhimu kwa viongozi wa Ulaya kujadili juu ya hatua nzuri na zenye ufanisi na zile zisizo na tija, akiongeza kuwa "sisi nchini Ujerumani, kwa vyovyote vile, tuna mtazamo kwamba kufungwa kwa mipaka siyo jibu stahiki kwa changamoto hii."
Ujerumani siyo jirani wa moja kwa moja na Italia, ambayo ndiyo kitovu cha mripuko huo barani Ulaya. Austria na Slovenia zilizoko kaskazini mwa Italia, na Malta upande wa kusini, zimefunga kwa sehemu kubwa mipaka yake na Italia. Merkel pia ameelezea huruma yake kwa raia wa taifa hilo ambalo wakaazi wake wote hawaruhusiwi kutoka eneo moja kwenda jingine.
"Ripoti kutoka huko, ushuhuda wa madaktari na wahudumu wa afya wanaofanyakazi kwa bidii, zinatuhuzunisha na pia tunawahurumia watu na viongozi wa kisiasa nchini Italia na tunawatakia kutoka moyoni, kwamba hatua ngumu walizozichagua kwa nchi zitaleta mabadiliko mazuri," alisema Merkel.
Italia yatangaza euro bilioni 25 kukabiliana na mripuko
Serikali ya Italia imetangaza kuwa inatenga kiasi cha euro bilioni 25 kukabiliana mripuko huo, ambapo matumizi ya kwanza yatafanyika kufikia mwisho wa wiki hii. Waziri wa uchumi Roberto Gualtieri amesema amri ya rais inayotarajiwa kufikia Ijumaa itaainisha matumizi ya karibu euro bilioni 12. Yatahusisha hatua za kusaidia idara ya afya na ulinzi wa kiraia na pia soko la ajira, kuhakikisha kuwa hakuna anaepoteza ajira yake baada ya virusi hivyo kuanza kupunguza uzalishaji wa viwandani.
Kansela Merkel amesema wakati huo, kuwa kulingana na makadirio ya wataalamu asilimia hadi 70 ya raia wa Ujerumani wanaweza kuathiriwa na virusi vya corona, akisisitiza kuwa hatua zinazochukuliwa zinapaswa kuelenga kupunguza kasi ya kuenea kwake.
Nchini Iran idadi ya vifo kutokana na virusi hivyo imepanda kwa siku ya pili mfululizo baada ya kuripotiwa vifo 62 katika muda wa saa 24, na kufikisha jumla ya watu waliokufa nchini kuwa 354. Iran inashika nafasi ya tatu miongoni mwa nchi zilizoathirika zaidi ya mripuko huo baada ya China yenye idadi kubwa zaidi ya vifo 3,158 na Italia ambayo mpaka sasa imerikodi vifo zaidi ya 460.
Wengi wanapona
Kwa watu walio wengi, kirusi hicho kipya kinasababisha ishara za wastani, kama vile homa na kikohozi. Kwa baadhi, hasa wenye umri mkubwa na watu wenye matatizo ya kiafya, kinaweza kusababisha maradhi makali, ikiwemo homa ya mapafu.
Asilimia kubwa ya watu hupona kutokana na virusi hivyo na kwa mujibu wa shirika la afya dunia, watu wenye ugonjwa usio mkali hupona katika muda wa karibu wiki mbili, huku wale wenye ugonjwa mkali huweza kuchukua kati ya wiki tatu na sita kupona.
Chanzo: Mashirika