CPJ: Waandishi wadhalilishwa Uganda kipindi cha corona
23 Aprili 2020Kulingana na waandishi wenyewe na Mtandao wa Haki za Waandishi wa Habari Uganda, tangu Machi 19 karibu waandishi sita wameshambuliwa na maafisa wa usalama wa Uganda wakati walipokuwa kazini kuripoti kuhusu jinsi maafisa hao walivyokuwa wakitekeleza amri zilizotolewa kwa ajili ya kupunguza maambukizi ya virusi vya corona.
Muthoki Mumo ni mwakilishi wa CPJ katika nchi za Afrika zilizo kusini mwa jangwa la Sahara.
"Rais Yoweri Museveni alisema kwamba waandishi Uganda ni miongoni mwa watu wanaofanya shughuli muhimu, kwa hiyo inatia wasiwasi sana kuona walinda usalama na wanajeshi wakiwashambulia waandishi licha ya uwepo wa amri hii" alisema Muthoki Mumo.
Polisi walijaribu kumkamata ila alikataa
Mnamo Machi 19 katika wilaya ya kaskazini ya Kitgum maafisa wa polisi walimpiga makofi, ngumi na mateke Julius Ocungi ambaye ni mkuu wa shirika la habari la mtandao wa redio Uganda. Ocungi aliiambia CPJ kwamba alipokea kipigo hicho alipokuwa akipiga picha tukio la polisi kuifunga baa moja kama sehemu ya kutekeleza amri ya rais.
Maafisa watatu wa polisi walijaribu kumkamata ila alikataa na kuondoka eneo hilo ingawa waliichukua kamera yake na baadae siku hiyo hiyo alipokwenda kituoni kuichukua, maafisa hao walimtaka azifute picha alizopiga ila alikataa.
Na Machi 30 wanajeshi waliokuwa wamevaa nguo za kiraia walimvamia mwandishi wa redio moja iitwayo Redio Apac kaskazini mwa Uganda, Denis Okello. Kulingana na mwandishi huyo, watu watatu walimfuata na kuanza kumpiga wakati alipokuwa amesimama kwenye ukumbi wa kituo hicho cha redio. Walijaribu kumuamuru aende nao katika kituo cha polisi ila alikataa.
Kulingana na Mumo, visa walivyovinakili ni vichache tu ila waandishi wengi wanapitia wakati mgumu mikononi mwa polisi katika kipindi hiki cha mapambano dhidi ya virusi vya corona.
Kamatakamata imeshuhudiwa nchi nyingine pia mbali na Uganda
Afisa huyo wa CPJ anadai wakuu wa usalama waliowasiliana nao Uganda wamesema wanayachunguza matukio hayo ila ameeleza pia si waandishi wa Uganda pekee wanaopitia magumu.
"Tumenakili kamatakamata ya waandishi Somalia na Ethiopia. Kwa sasa tunafanya uchunguzi ili kubaini chanzo cha visa ambavyo vimeripotiwa kwetu kutoka Rwanda, Tanzania na hata Kenya. Kuhusu Rwanda bado tunachunguza kwa sababu tuna wasiwasi kuhusiana na ripoti za waandishi waliokamatwa," alisema Muthoki Mumo.
Rais Paul Kagame wa Rwanda hivi majuzi aliripotiwa kutoa kauli iliyoonekana kuelekezewa waandishi wa habari akisema hakuna atakayewatetea katika kipindi hiki cha mapambano dhidi ya virusi vya corona.