1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Cuba kupata rais mpya

19 Aprili 2018

Rais Raul Castro wa Cuba anastaafu na kukabidhi madaraka kwa makamu na mtu wake wa karibu, Miguel Diaz-Canel, lakini wengi wanaona mabadiliko haya hayana maana ya kubadilisha mfumo wa kisiasa na kiuchumi.

https://p.dw.com/p/2wJKl
Kuba Vizepräsident Miguel Diaz-Canel
Picha: Reuters/A. Ernesto

Bunge nchini Cuba linakutana kumteua rais mpya wa Baraza la Taifa ambaye atakuwa pia rais wa nchi hiyo ya kisoshalisti ya Amerika Kusini. Hatua hii inayohitimisha miaka 10 ya Raul Castro imepokewa kwa mchanganyiko wa matumani ya kufunguka zaidi kwa taifa hilo na pia fadhaa hasa kutokana na mahusiano yanayozidi kuharibika na Marekani. 

Wiki iliyopita, Raul Castro alikosa nafasi adhimu ya kuaga kwenye jukwaa la kimataifa. Hakuwepo kwenye picha ya pamoja ya wakuu wa mataifa ya Amerika. Mkuu huyo wa chama cha Kikomunisti kinachoitawala Cuba alikuwa amemtuma waziri wake wa mambo ya kigeni kwenye mkutano huo wa kilele uliofanyika mjini Lima, Peru. 

Rais Donald Trump wa Marekani naye pia alijitenga kando, na kwa hivyo pasingekuwapo na kupeana mikono kwa viongozi wa mataifa mawili kama ilivyotokea mwaka 2015, ambapo Castro alikutana na rais wa zamani wa Marekani, Barack Obama na kwa mara ya kwanza wakayaleta mataifa yao karibu zaidi kwa kupeana mikono na kupiga picha ya pamoja.

“Bali hatupaswi kujipotosha wenyewe. Tunatenganishwa sana. Historia baina ya nchi zetu mbili imekuwa ngumu. Lakini sasa tuko tayari kuanzisha urafiki baina ya watu wetu, tuko tayari kuzungumzia yote, kwa kuvumiliana,” alisema Castro, ambaye sasa anaachia madaraka akiwa na umri wa miaka 86.

Hakuna matumaini ya mabadiliko ya mfumo wa kisiasa, kiuchumi

Hata hivyo, baada ya takribani miaka 60 ya utawala wa akina Castro, mabadiliko ya sasa ya uongozi hayatazamiwi kuleta mageuzi makubwa kwenye uchumi wa taifa hilo la visiwa lenye mfumo wa chama kimoja cha siasa.

Kuba Raúl Castro und Miguel Díaz-Canel
Miguel Díaz-Canel (kulia) anachukuliwa kama mtu wa karibu sana wa Raúl Castro.Picha: Getty Images/AFP/J. Beltran

Makamu wa Rais Diaz-Canel, mwenye umri wa miaka 57, anaonekana kama kada wa Chama cha Kikomunisti, kinachopewa jukumu la kuwa nguvu pekee ya kisiasa na katiba ya Cuba. Mrithi huyu wa urais amekuwa sehemu ya chama hicho kwa zaidi ya miongo mitatu.

Hata kama anaondoka madarakani, Raul Castro ataendelea kuwa na nguvu kubwa, kwani anabakia kuwa mkuu wa chama tawala hadi mkutano mkuu utakapofanyika mwaka 2021. 

Wakati wabunge wakikutana saa tatu asubuhi kwa majira ya Cuba kutangaza matokeo ya kura zao kwa uchaguzi wa Diaz-Canel, ambaye hana mpinzani, kwa wengi wanaopambana na hali ngumu za kimaisha nchini Cuba, ubadilishanaji huu wa madaraka ya uongozi wa juu unaonekana kama jambo la kupitisha muda tu.

Hilo, hata hivyo, halitaondosha ukweli kwamba hakuna mapinduzi yoyote ya Amerika Kusini yaliyofanikiwa kulitikisa bara hilo kuliko mapinduzi ya Cuba chini ya akina Castro, ambao sasa wanahitimisha utawala wao.

Mwandishi: Mohammed Khelef/Emilia Ramos
Mhariri: Josephat Charo