Ramaphosa aahidi kupambana na rushwa
17 Februari 2018
Akilihutubia taifa kupitia bunge la nchi hiyo na huku akipigiwa makofi na kushangiliwa Ramaphosa alitoa mwito kwa wananchi wa Afrika Kusini kuweka kando tofauti zote miongoni mwao ambazo zimeliathiri taifa hilo na kuanza sasa mwanzo mpya.
Mwanzoni mwa hotuba yake Ramaphosa alimsifia mtangulizi wake Jacob Zuma kwa utendaji wake kwa taifa na kuibua sauti za miguno kutoka kwa baadhi ya wabunge. Hata hivyo Zuma hakuwepo bungeni wakati wa hotuba hiyo hapo jana.
Ramaphosa ambaye alikuwa makamu wa rais chini ya utawala wa rais Jacob Zuma amesema utawala wake utajikita zaidi katika kutengeneza ajira pamoja na kuvutia uwekezaji na kwamba ni muda muafaka sasa kwa taasisi za umma pamoja na viongozi kurejesha imani iliyokuwa inaanza kutoweka.
Amesema mwaka huu serikali yake itapambana na vitendo vya rushwa katika taasisi za umma na kuongeza kuwa idara zinazohusika na kuzuia vitendo vya uhalifu zimekuwa zikichukua hatua ambazo zitasaidia kupambana ipasavyo na rushwa.
Ramaphosa ambaye wakati wa hotuba hiyo alionekana kuwa mtulivu na mwenye bashasha alisema tume maalumu kwa ajili ya kufanya uchunguzi katika taasisi mbalimbali inatarajia kuanza kazi yake hivi karibuni na kuwa wote wanaohusika na vitendo vya kifisadi watafichuliwa.
Wanachi Afrika Kusini waonesha matumaini kwa Ramaphosa
Walio wengi nchini Afrika Kusini wanamatumaini kuwa Ramaphosa mmoja wa wanaharakati wa ukombozi wa taifa hilo kutoka kwa utawala wa wazungu wachache ataleta mageuzi nchini humo baada ya kukithiri kwa kashfa za rushwa, ambazo zimepunguza umaarufu wa chama tawala cha African National Congress (ANC).
Miongoni mwa tuhuma zilizokuwa zikimuandama mtangulizi wa Ramaphosa, Jacob Zuma, ni pamoja na kuruhusu familia ya wafanyabiashara maarufu nchini humo ya Gupta kujipatia mikataba mikubwa ya kibiashara na pengine hata familia hiyo kushawishi uteuzi wa nafasi kadhaa katika baraza la mawaziri nchini humo.
Julius Malema kiongozi wa chama cha upinzani cha Economic Freedom Fighters alisema baada ya hotuba hiyo kuwa anakaribisha baadhi ya ahadi za Ramaphosa zinazohusiana na kupambana na rushwa na kuongeza kuwa walikuwa na tatizo na kiongozi aliyepita akimaanisha Zuma na kuwa sasa tatizo limeondoka.
Zuma ambaye anaweza akakabiliwa na mashtaka alionekana kutojali hadi wakati alipojiuzulu Jumatano wiki hii huku akisema hatambui kosa alilofanya.
Katika siku chache tangu Jacob Zuma kujiuzulu polisi wamewakamata watu kadhaa wanaodaiwa kuhusika na ufisadi katika mashirika ya umma na mmoja wa watendaji wakuu katika shirika linalotoa huduma ya umeme linalomilikiwa na serikali, ambaye pia alikuwa akichunguzwa, amejiuzulu.
Mwandishi: Isaac Gamba-dpae/ape
Mhariri: Yusra Buwayhid