Daktari Mukwege atajwa kuwa shujaa
24 Oktoba 2014Taarifa iliyogongwa vichwa vya habari wiki hii duniani kote ni kusambaa kwa kasi kwa ugonjwa wa Ebola. Na hata hapa Ujerumani kumekuwa na taarifa nyingi pamoja na makala zinazoelezea mapambano dhidi ya ugonjwa huo. Zipo habari nyingi za visa vya wale walioambukizwa virusi vya Ebola au watu waliojitolea kuwahudumia. Katika gazeti la "der Freitag" ipo habari kuhusu muuguzi kutoka Norway aliyekwenda Sierra Leone kuwasaidia wagonjwa wa Ebola.
Anine Kongelf ni nesi mwenye miaka 27. Amejiunga na shirika la msalaba mwekundu nchini Sierra Leone kupambana na Ebola. Ameshuhudia watu wengi wakipoteza maisha yao. Lakini leo ni siku ya bahati. Baada ya kupata matibabu, msichana Kadiatu mwenye miaka 11 na Osman mwenye miaka 35 wamepona na sasa wameruhusiwa kwenda nyumbani. Anine anasema ni visa kama hivyo vinavyompa matumaini kwamba ugonjwa wa ebola unaweza kushindwa.
Cuba yatoa mchango mkubwa
Katika gazeti la "Frankfurter Allgemeine Zeitung" tunakutana na habari ya wauguzi kutoka Cuba ambao nao wameamua kujiunga na mapambano dhidi ya Ebola. Cuba ilikuwa miongoni mwa nchi za kwanza kutuma msaada na wasaidizi Afrika Magharibi, baada ya Ebola kulipuka. Ni hatua iliyosifiwa sana na Shirika la Afya Duniani na Umoja wa Ulaya. Hata Marekani, mahasimu wakubwa wa Cuba, wamesema huu ni mfano wa kuigwa.
Mwanzoni mwa Oktoba mwaka huu, madaktari na wauguzi 165 kutoka Cuba waliwasili katika mji mkuu wa Sierra Leone, Freetown. Wiki hii, Cuba iliamua kutuma timu nyingine ya wataalamu 300 wa afya kwenda Liberia na Guinea. Cuba ina historia ndefu ya kutuma madaktari wake nchi za nje. Tangu baada ya mapinduzi ya mwaka 1959, nchi hiyo imekuwa mstari wa mbele katika kuwahudumia watu kwenye nchi za kimaskini huko Amerika ya Kusini na Afrika, mara nyingi, bila gharama yoyote.
Wanawake 40,000 wametibiwa
Mbali na habari za ebola, wiki hii kulikuwa pia na taarifa nzuri kutoka Afrika. Ni habari ya daktari Denis Mukwege wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, aliyepewa tuzo ya haki za binadamu ya Bunge la Umoja wa Ulaya.
Gazeti la Frankfurter Allgemeine Zeitung limechapisha taarifa inayoelezea maisha ya daktari huyo mwenye miaka 59 na harakati zake za kuwatibu wanawake na watoto waliobakwa. Mwandishi wa makala hiyo anasema: Kwa wanawake wa Kongo, Denis Mukwege amekuwa tumaini na msaada mkubwa. Daktari huyo ni mtaalamu wa kuwatibu wanawake waliobakwa kikatili kabisa, wakati mwingine hata kwa kutumia chupa au bunduki. Wengi wanaokuja hospitalini kwake wamebakwa zaidi ya mara moja.
Kila siku wanawake wasiopungua 10 wanafika kwenye hospitali ya Panzi inayoendeshwa na daktari huyo. Katika miaka 16 iliyopita, Mukwege na timu yake wamewafanyia upasuaji wanawake 40,000 kuziunda upya sehemu za siri za wanake hao walionyajisiwa. Tuzo ya haki za binadamu ya Bunge la Ulaya ni moja ya zawadi nyingi alizopokea daktari huyo katika miaka iliyopita.
Hata gazeti la Berliner Zeitung limeandika makala kuhusu daktari huyo. Makala hiyo inaanza na nukuu kutoka kwenye kitabu cha mwandishi wa habari Eve Enseler wa Marekani aliyeitembelea hospitali ya daktari huyo na kuelezea kile alichokishuhudia. Enseler anaandika: "Nitawezaje kumwelezea msichana wa miaka 9 aliyebakwa na kundi zima la wanajeshi?" Enseler ameifananisha hospitali ya daktari Mukwege na jehanamu, kwa sababu ya unyama waliofanyiwa wanawake na wasichana wanaotibiwa hapo.
Makala hiyo inaendelea kusema: Licha ya msaada anaoutoa kwa jamii, baadhi ya Wakongo wanamuona Mukwege kama adui. Mwaka 2012, watu wasiojulikana walimvamia nje ya nyumba yake. Dereva wa Mukwege aliuliwa, yeye mwenyewe na familia yake waliponea chupuchupu. Mukwege alikwenda uhamishoni Ulaya. Lakini sasa amerudi na anaendelea kufanya kazi katika hospitali yake.
Mwandishi: Elizabeth Shoo
Mhariri: Saumu Yusuf