Daktari wa Michael Jackson atiwa hatiani kwa mauaji
8 Novemba 2011Mamia ya waungaji mkono wa Michael Jackson walishangiria kwa furaha wakati maamuzi hayo ya mahakama ya Los Angeles, yakisomwa:
"Katika kesi kati ya watu wa California wakiwa walalamikaji na Conrad Murray akiwa mshtakiwa, kesi nambari FA 073164, sisi jopo la majaji katika kesi hii, tumemuona mshtakiwa Conrad Murray ana hatia ya kumuuwa bila kukusudia Michael Joseph Jackson tarehe 25 Juni 2009, ikiwa ni kinyume na Sheria ya Jinai Kifungu 192, kifungu kidogo cha B."
Dakika chache baadaye, jaji Michael Pastor aliamuru daktari huyo mwenye miaka 58 atiwe pingu na apelekwe rumande, kusubiri hukumu rasmi mwishoni mwa mwezi huu.
Mama mzazi wa Jackson, Katherine, alilia huku akikumbatiwa na mtoto wake, Jarmaine, mmoja wa kaka wa Michael. Murray ametiwa hatiani kwa kumpa dozi kubwa Michael ambayo alikusudia kumsaidia kupata usingizi, baada ya nyota huyo wa muziki wa pop, kufanya mazoezi makali kwa ajili ya onyesho lake lililotarajiwa kuwa la aina yake, miaka mitatu iliyopita.
Mwenyewe Murray alikiri kumpa Jackson kiwango kidogo cha dawa aina ya propofol, lakini sio kama kilichogundulika kwenye mwili wa nyota huyo baada ya kufariki.
Akizungumzia hukumu hii, Jarmeine amesema na hapa namnukuu: "Haki imetendeka. Hakuna kitakachomrudisha Michael duniani, lakini tumefurahi kwamba Murray amekutikana na hatia." Mwisho wa kumnukuu.
Dada yake Michael aitwaye La Toya, aliandika kwenye mtandao wa Twitter, kwamba huu ni ushindi, na familia yao inaishukuru timu ya mwanasheria wa serikali, David Walgren, kwa kuipatia haki yake.
Katika ufungaji wa hoja zake wiki iliyopita, wakili wa upande wa mashitaka, Walgren, alimtuhumu Murray kwamba alisababisha kifo cha Michael Jackson kwa sababu ya uzembe na uroho, na hivyo kuwanyima watoto wa nyota huyo baba yao na kuinyima dunia, mtu mwenye kipaji na akili nyingi.
Kwa upande wake, wakili wa utetezi, Ed Chernoff, alihoji kwamba Michael Jackson alikuwa mlevi wa madawa, jambo ambalo lilisababisha kifo chake baada ya kunywa madawa mengine kadhaa wakati Murray akiwa hayumo chumbani. Wakili huyo alimfananisha mteja wake na samaki mdogo kwenye dimbwi kubwa na chafu, akiwatuhumu mashahidi kwa kuzusha hadithi ya kubuni baada ya kifo cha Michael Jackson.
Hata hivyo, muda mfupi kabla ya maamuzi ya jopo la majaji kusomwa, daktari wa zamani wa Michael Jackson alivunja ukimya wake wa siku nyingi, kwa kusema kwamba nyota huyo hakuwa mlevi wa madawa, wala hakuwahi kumpiga sindano nyingi za kuzuia maumivu.
Akiwa na uso wenye fadhaa, Murray hakusema chochote baada ya maamuzi dhidi yake kusomwa. Sasa daktari huyo mwenye asili ya visiwa vya Carrebean, anakabiliwa na kifungo cha hadi miaka minne jela na pia kunyang'anywa leseni yake ya udaktari nchini Marekani.
Tayari jimbo la California limeshaizuia leseni yake, wakati majimbo ya Nevada na Texas yakisema yanasubiri hukumu kamili. Wakili wake hajasema ikiwa mteja wake atakata rufaa ama la.
Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP/Reuters
Mhariri: Oummilkheir Hamidou