DAMASCUS : Katibu Mkuu Annan akutana na Rais Assad
1 Septemba 2006Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Kofi Annan amesema amepatiwa hakikisho kutoka kwa Rais Bashar al Asaad wa Syria kwamba serikali ya Damascus itachukuwa hatua zote zinazohitajika kusaidia utekelezaji wa azimio la Umoja wa Mataifa kwa Lebanon.
Kufuatia mazungumzo yake na rais huyo wa Syria mjini Damascus Annan amesema kiongozi huyo wa Syria ameahidi kuimarisha doria za mpakani na kushirikiana na jeshi la Lebanon kuzuwiya upelekaji wa silaha kwa Hizbollah.Annan pai ameitaka Syria kutumia ushawishi wake kusaidia kuachiliwa huru kwa wanajeshi wa Israel wanaoshikiliwa mateka na Hizbollah nchini Lebanon na wanamgambo wa Kipalestina huko Gaza.
Assad hakuzungumzia kitu hadharani juu ya mkutano wao huo lakini Annan alizungumza hayo na waandishi wa habari katika uwanja wa ndege wa Damascus kabla ya kuelekea Qatar.
Katibu Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa anakamilisha ziara yake ya Mashariki ya Kati nchini Iran hapo kesho.