Daraja muhimu kwenda Tigray laharibiwa Ethiopia
2 Julai 2021Shirika la misaada ya kiutu la International Rescue Committee limesema kuharibiwa kwa daraja kwenye Mto Tekeze kutahujumu zaidi juhudi za kupeleka misaada kwenye jimbo la Tigray.
Mkoa huo unaokumbwa na machafuko ni moja ya maeneo yanayokabiliwa na njanga la kibinaadamu ulimwenguni. Marekani ilisema zaidi ya watu laki tisa kwenye mkoa wa Tigray wamekumbwa na baa la njaa.
''Umeme na mawasiliano bado vimekatwa''
Haijafahamika wazi ni nani aliyehusika na kubomowa daraja hilo kwenye barabara kuu ya magharibi mwa Tigray, eneo linalokaliwa na vikosi kutoka jimbo jirani la Amhara. Msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Eri Kaneko, amesema hali kwenye mji mkuu wa Tigray, Mekelle, bado ni tete.
''Umeme na mawasiliano bado vimekatwa kwenye mkoa huo. Hakuna ndege au barabara ya kuingia au kutoka kwenye eneo hilo.''
Mkuu wa shirika la misaada ya maendeleo la Marekani,USAID, Samantha Power, alisema kwenye mtandao wake wa Twitter kuwa kuharibiwa kwa daraja hilo ni balaa.
Kikao cha dharura cha Umoja wa Mataifa
Balozi wa Ufaransa kwenye Umoja wa Mataifa, Nicolas De Riviere, ambaye nchi yake inaongoza Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa mwezi huu wa Julai, amesema Baraza hilo litaitisha kikao leo Ijumaa kujadili hali ya kisiasa na ya kiutu kwenye mkoa wa Tigray.
Mashirika ya misaada yamekuwa yakifuatilia taarifa kuhusu madaraja mengine muhimu ambayo yameripotiwa pia kuharibiwa. Aidha, viongozi wa Ethiopia walipiga marufuku ndege za kigeni kuruka chini ya futi 29 elfu kwenye anga ya mkoa wa Tigray, kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mamlaka ya Usafiri wa Anga ya Marekani.
Ethiopia yawataka waasi kuheshimu usitishaji mapigano
Wakati huo huo, Ethiopia imewatolea wito waasi wa TPLF huko Tigray kuheshimu amri ya kusitisha mapigano iliyotangazwa na serikali. Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Ethiopia, Dina Mufti, amewaambia waandishi habari kwamba ingawa uamuzi wa kusitisha mapigano ulikuwa wa upande mmoja, lakini utekelezaji wake unahitaji pia utiifu kutoka upande wa waasi.
Tangazo hilo la kusitishwa mapigano la siku ya Jumatatu lilitolewa baada ya wanajeshi wa serikali kuondoka Mekelle ambao ni mji mkuu wa jimbo la Tigray na kuruhusu wanajeshi wa vikosi vya ulinzi vya Tigray, TDF, kuingia jimboni humo.
Hata hivyo, msemaji wa TDF aliutaja uamuzi wa kusitisha mapigano uliotangazwa na serikali kuwa "kichekesho" na kwamba wapiganaji wa TDF walishadhamiria kuwafukuza wanajeshi wote wa serikali kuu ya Ethiopia pamoja na washirika wao.