David Moyes kuiongoza Manchester United
10 Mei 2013Ushawishi wa Fergie katika klabu ya Man United utaendelea hata baada ya kustaafu kutoka wadhifa huo. Hii ni baada ya mabingwa hao wa Premier League kuzingatia ushauri wake na kumchagua David Moyes kama mkufunzi mpya atakayevaa viatu vya Sir Alex.
Moyes ambaye atajiuzulu kama kocha wa Everton mwishoni mwa msimu huu baada ya kuiongoza klabu hiyo kwa miaka 11 alipigiwa upatu kuchukua nafasi ya Fergie ambaye anatoka Scotland kama yeye katika klabu ya United, na amesaini mkataba wa miaka minne kuanzia Julai mosi. Ferguson amesema wamewajadili wagombea wa nafasi hiyo na wakamchagua kwa kauli moja David Moyes. Fergie atasalia kama balozi na mkurugenzi wa klabu hiyo ya Old Trafford.
Naam na bila shaka macho yote yataelekezwa katika viwanja vya Manchester United na Goodison Park kesho Jumapili wakati Ferguson na Moyes watakapowaaga mashabiki wao wa nyumbani. Manchester United itacheza dhidi ya Swansea wakati Everton ikiwa mwenyeji wa West Ham.
Lampard kuhusu Mourinho
Kulikuwa na majina kadhaa yaliyokuwa yakipigiwa upatu kuchukua nafasi ya Freguson, na Jose Mourinho ni mmoja wa wakufunzi waliokuwa kwenye orodha hiyo. Ripoti za karibuni za vyombo vya habari nchini Uhispania na Uingereza zilisema kuwa kocha huyo wa Real Madrid anatathmini kuondoka klabu hiyo mwishoni mwa msimu huu na kurudi katika uwanja wa Stamford Bridge. Kuhusiana na hilo, kiungo wa Chelsea na naibu nahodha Frank Lampard amesema kuwa hizo ni habari njema kwa klabu hiyo nzima kama litafanyika. Lampard amesema awali amesikia kuhusu uvumi wa aina hiyo lakini mwishowe hutokea kocha mwingine hivyo basi bado haijajulikana kama ripoti zinazohusu Mourinho ni za msingi. Mkataba wa Lampard mwenye umri wa miaka 34 na mabingwa hao wa Ulaya unakamilika mwishoni mwa msimu huu, na hakuna dalili za kuwa ataongezewa msimu ujao…Mourinho aliiongoza Chelsea kwa ushindi wa mataji mawili ya Premier League katika kipindi chake cha miaka mitatu kuanzia mwaka 2004-2007 kabla ya kuhamia Inter Milan na kisha Real Madrid.
Bayern kukabidhiwa Ngao ya Bundesliga
Bayern Munich wamekabidhiwa leo taji lao la kwanza baada ya miaka mitatu ya ukame. Bayern wameinyanyua ngao ya Bundesliga ya msimu huu na mwenyekiti Karl-Heinz Rummenige amesisitiza hilo halitakuwa kombe la mwisho watakalotwaa msimu huu.
Miamba hao sasa wameangazia macho katika fainali ya kukata na shoka dhidi ya Borussia Dortmund ya Champions League uwanjani Wembley, London mnamo Mei 25. Hiyo itakuwa fainali ya tatu ya Bayern katika Champions League ndani ya misimu minne huku Rummenige akisisitiza kuwa wamejifunza makosa waliyofanya wakati wa kichapo cha Chelsea mwaka jana na Inter Milan mwaka wa 2010.
Mashabiki wamevalia nguo za kitamaduni katika mitaa ya Bavaria hapa Ujerumani, kusheherekea ushindi wa taji lao la 22 wakati klabu hiyo ikiandaa gwaride la wachezaji wake bora kabisa 22 waliowahi kuichezea klabu hiyo katika siku za nyuma. Magwiji hao ni kama vile Gerd Mueller, Franz Beckenbauer, Lothar Matthaeus, Paul Breitner, Oliver Kahn na Bixente Lizarazu.
Thomas Bach ataka wadhifa wa rais IOC
Mjerumani Thomas Bach ndiye mgombea wa kwanza rasmi kujitokeza kumrithi Jacque Rogge kama rais wa Kamati ya Kimataifa ya Michezo ya Olimpiki – IOC. Bach mwenye umri wa miaka 59, ambaye ni makamu wa rais wa IOC, ametangaza nia hiyo mjini Frankfurt kugombea urais wa kamati ya Olimpiki. Rogge, ambaye alimrithi Juan Antonio Samaranch mnamo mwaka wa 2001 anajiuzulu Septemba 10 baada ya kuwa uongozini kwa miaka 12. anatarajiwa kupambana na wagombea wengine kadhaa ikiwa ni pamoja na Ng Set Miang kutoka Singapore. Ni makamu rais wa IOC ambaye aliongoza kamati andalizi kwa michezo ya mwanzo ya olimpiki kwa vijana nchini Singapore mwaka wa 2010. mwingine ni Richard Carrion kutoka Puerto Rico, ambaye ni mwenyekiti wa Tume ya Fedha ya IOC.
Muda wa mwisho wa kutangaza nia ya kugombea ni Juni 10. rais mpya atachaguliwa katika kikao cha Kamati ya Olimpiki mjini Buenos Aires, Argentina mnamo Septemba 10.
Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA
Mhariri: Abdul-Rahman