DAVOS: Kansela Merkel na rais Abbas wakutana Uswissi
26 Januari 2007Kansela wa Ujerumani,Angela Merkel amekutana na rais wa Wapalestina,Mahmoud Abbas pembeni mwa mkutano wa uchumi duniani,mjini Davos,Uswissi. Baadae,Abbas aliwaambia waandishi wa habari anataraji kuwa Ujerumani ambayo hivi sasa imeshika wadhifa wa urais wa Umoja wa Ulaya,itajihusisha zaidi katika suala la Mashariki ya kati.Kansela Merkel nae amesema, Umoja wa Ulaya utashughulikia zaidi utaratibu wa amani katika Mashariki ya Kati.Akaongezea kuwa umoja huo katika kundi la pande nne-ikiwa ni pamoja na Marekani,Urussi na Umoja wa Mataifa, utaweza kutoa mchango muhimu.Rais Abbas alikutana pia na waziri wa kigeni wa Israel Tzipi Livni na wote wawili wamekubaliana kuwa amani ya kudumu katika Mashariki ya Kati itaweza tu kupatikana ikiwa wafuasi wa siasa kali kutoka pande zote mbili watanyangywa silaha.