1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Dimba la Afrika latarajiwa Gabon lakini hakuna msisimko

5 Januari 2017

Mizozo ya kijamii, kiuchumi na kisiasa imetamba nchini humo na kupotezea baadhi ya raia hamu ya dimba hilo linalotarajiwa

https://p.dw.com/p/2VLK8
Africa Cup Burkina Faso vs Gabun Aubameyang 17.01.2015
Picha: De Souza/AFP/Getty Images

Zimesalia siku chache tu kabla ya dimba la kombe la Afrika, kuanza nchini Gabon. Mshambuliaji Pierre-Emerick Aubameyang anayesakata soka ya kulipwa nchini Ujerumani anatarajiwa kuongoza nchi yake ambayo ndio wenyeji kutwaa kombe hilo. Hata hivyo, hali ya hisia imeendelea kuwa baridi na bila msisimko. 

Katika barabara za mji mkuu Libreville, yapo mabango yaliyopambwa na yakitangaza kinyang'anyiro hicho. Kinyang'anyiro kinachotarajiwa kuanza rasmi tarehe 14 mwezi huu na kuendelea hadi Februari 5.

Kwenye miji mingine ambapo mechi zitachezwa mfano, Oyem ulioko Kaskazini, Francevile ulioko kusini mashariki na Port-Gentil ambao ndio makao makuu ya uzalishaji wa mafuta, juhudi hizo za mwisho mwisho zimeshika kasi, kuhakikisha viwanja vitakavyotumika viko sawa.

Kikosi cha Gabon kinaongozwa na mshambuliaji matata wa kulipwa anayechezea timu ya Borussia Dortmund nchini Ujerumani Aubameyang na pia mchezaji wa kiungo cha kati wa timu ya Juventus Mario Lemina na Didier Ndong anayechezea Sunderland.

Hata hivyo, nchi hiyo ndogo ya Afrika ya Kati imesalia kuwa katikati ya mizozo ya kijamii na kisiasa. Raia hawajashawishika kikamilifu kufurahia mechi. ''Akili zetu haziko katika kandanda''. Amesema Stephane Mba mkaazi wa Libreville

Wachezaji wa Zambia wakisherehekea ushindi wao wa CAN mwaka 2012
Wachezaji wa Zambia wakisherehekea ushindi wao wa CAN mwaka 2012Picha: Getty Images/AFP/F. Fife

Mafuta ndiyo tegemeo kuu la uchumi wa nchi hiyo yenye jumla ya watu milioni 1.8 kando na kuwa na idadi kubwa ya wahamiaji kutoka Senegal, Burkina Faso na Cameroon. Hata hivyo nchi hiyo imeathiriwa na mzozo mkubwa wa kiuchumi kufuatia kuporomoka kwa bei ya mafuta. Hali ambayo imesababisha unyonge na ukosefu wa msisimko kwa raia.

Akitoa hotuba yake ya kufungua mwaka 2017, Rais wa Gabon, Ali Bongo Ondimba, alikiri kuwa raia wengi nchini mwake kwa sasa wanakumbwa na changamoto. Wengi wa watu wetu wameathiriwa sana na mizozo ya kiuchumi inayokumba ulimwengu. Nafasi nyingi za ajira zimepotea hasa katika sekta ya mafuta. Alisema Bongo.

''Miji ya Libreville, Port-Gentil, Franceville na Oyem imepoteza sifa zao za uchangamfu na kupendwa na watu wapendao starehe na sherehe''. Ni maoni ambayo yamechapishwa katika gazeti la L'Union

Katika miezi ya hivi karibuni kumekuwa na wito wa kufanywa migomo hasa miongoni mwa wafanyakazi wa umma. Kadhalika wito unazidi kuhanikizwa wa kutaka mabadiliko ya kisiasa.

Wanajeshi wakishika doria katika barabara za Libreville
Wanajeshi wakishika doria katika barabara za LibrevillePicha: Getty Images/AFP/S. Jordan

Takriban miezi sita imepita tangu kufanywa kwa uchaguzi mkuu, lakini kiongozi wa upinzani Jean Ping ameendelea kusema yeye ndiye alishinda uchaguzi huo wa urais na kuwataka Wagabon kupinga uongozi wa Bongo anaosema ni wa kidikteta.

Ushindi wa Rais Bongo mnamo mwezi Agosti na kuidhinishwa na mahakama ya kikatiba ulipingwa na vyama vya upinzani pamoja na Umoja wa Ulaya. Ushindi wake ulizua ghasia na mauaji kutokea.

Magazeti ya upinzani mara kwa mara yamewataka watu kususia michuani hiyo ya kombe la bara Afrika.

Raia wengine ambao wangali wanaathiriwa mawazo ya ghasia zilizotokea baada ya uchaguzi wanahofia huenda mechi hizo zikakumbwa na machafuko hasa miji pinzani ya  Port-Gentil na Oyemi.

Rais amejaribu kutuliza wasiwasi kwa kutilia msisitizo ahadi yake ya kuanzisha majadiliano ya kisiasa punde baada ya kukamilika kwa michuano hiyo, lakini Ping amekataa.

Hata hivyo, Rais Bongo anatumai kuwa mechi hizo zitaleta utulivu katika kipindi zitakapokuwa zikiendelea.

Mwandishi: John Juma/AFPE

Mhariri: Grace Patricia Kabogo