Dirisha la uhamisho la Bundesliga 2022
Ripoti kutoka Ujerumani na Uingereza zinaashiria kwamba uhamisho wa Sadio Mané kutoka Liverpool kwenda Bayern Munich unakaribia kukamilishwa. Limekuwa dirisha lenye shughuli nyingi kwa Bayern hadi sasa.
Sadio Mané (Liverpool → Bayern Munich)
Usajili unaokaribia wa mshambuliaji nyota wa Senegal wa Liverpool ni mapinduzi ya kweli kwa Bayern Munich na pia kwa Bundesliga, ligi ambayo imekuwa ikishuhudia wachezaji wa juu wakielekea katika timu pinzani kwa Ligi ya Premier. Kwa €32m, ambayo inaweza kupanda hadi €41m, kwa mabao yake (120 katika mechi 269 alizoichezea Liverpool) yanaweza kusaidia kuchukua nafasi ya Robert Lewandowski.
Erling Haaland (BVB → Manchester city)
Baada ya miaka miwili na nusu katika klabu ya Dortmund, fundi wa mabao wa Norway anachukua hatua isiyoepukika hadi Ligi ya Premier, kwa Manchester city, ambapo baba yake Alf Inge aliwahi kucheza. Akiwa ametia kimyani mabao 85 katika michezo 88 kwa BVB, na kuchangia ushindi wa Kombe la Shirikisho la Ujerumani 2021, BVB watakuwa na kibarua kigumu kumtafuta atakayechukua nafasi yake.
Noussair Mazraoui (Ajax → Bayern Munich)
Kwa kumsajili beki wa kulia wa Ajax Mazraoui, mweye umri wa miaka 24, kocha wa Bayern Julian Nagelsmann ameweka tiki kwenye orodha yake ya ununuzi majira ya joto. Mchezaji huyo wa kimataifa wa Morocco mzaliwa wa Uholanzi alikuwa sehemu ya timu ya Ajax ambayo ilishinda mataji ya Eredivisie na anatarajiwa kuchukua nafasi ya Benjamin Pavard.
Ryan Gravenberch (Ajax → Bayern Munich)
Mchezaji wa Ajax, Ryan Gravenberch pia yuko njiani kuelekea Munich, mchezaji huyo mwenye miaka 20 akitarajiwa kuimarisha safu ya kati ya Bayern baada ya kusaini mkataba wa miaka mitano. "Ryan ni mchezaji wa kuvutia sana, kijana ambaye vilabu vingi vya juu vya Ulaya vingependa kumsajili," alisema Mkurugenzi Mtendaji wa Bayern Oliver Kahn.
Adam Hlozek (Sparta Prague → Leverkusen)
Akiwa bado na umri wa miaka 19, Adam Hlozek tayari ana misimu minne na Sparta Prague , mchezaji mwenye umri mdogo zaidi katika klabu hiyo. Alicheza mechi yake ya kwanza Novemba 10, 2018, akiwa na umri wa miaka 16 tu. Tangu wakati huo, amefunga mabao 40 katika michezo 105, pamoja na mechi 15 katika timu ya taifa ya Czech. Sasa yuko tayari kuungana na Patrik Schick huko Bayer Leverkusen.
Xaver Schlager (Wolfsburg → RB Leipzig)
Tayari ni mchezaji mashuhuri wa Bundesliga baada ya misimu mitatu akiwa na Wolfsburg, kiungo wa kati wa Austria aliyeimarika Schlager amesaini mkataba wa miaka minne na RB Leipzig. Baada ya kupitia katika klabu ya Red Bull Salzburg, mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 24 anafaa kusalia katika klabu dada ya Leipzig.
Alexander Schwolow (Hertha BSC → Schalke)
Baada ya kupata jeraha la msuli, mlinda mlango huyo mwenye umri wa miaka 30 alikosa mwisho wa msimu na akiwa benchi wachezaji wenzake wa Hertha Berlin walipambana kusalia kwenye Bundesliga kupitia mchujo. Mlinda mlango huyo wa zamani wa Freiburg anaweza kuwa na vita nyingine ya kushushwa daraja mikononi mwake kwa kuhamia kwa mkopo Schalke iliyopanda tena daraja.
Corentin Tolisso (Bayern Munich → unknown)
Mechi 118 ndani ya miaka mitano, sio matarajio ya Corentin Tolisso akiwa Bayern Munich. Mchezaji huyo wa kimataifa wa Ufaransa alisajiliwa kwa rekodi ya Bundesliga alipowasili kutoka Olympique Lyon kwa €41.5m mwaka 2017, lakini majeraha yamezuia maendeleo yake na kumzuia kufikia kiwango kinachohitajika Munich. Mkataba wa mchezaji huyo haujaongezwa tena, na yuko mbioni kutafuta klabu mpya.