Dissanayake ashinda uchaguzi wa urais nchini Sri Lanka
22 Septemba 2024Tume ya uchaguzi nchini Sri Lanka imemtangaza rasmi kiongozi anayeegemea siasa za kijamaa Anura Kumara Dissanayake kuwa mshindi wa uchaguzi wa urais na kumwangusha rais Ranil Wickremesinghe aliyemaliza muda wake. Taarifa ya Tume ya uchaguzi iliyochapishwa katika tovuti yake, imeonyesha kuwa Dissanayake mwenye umri wa miaka 55, alishinda kiti cha urais kwa asilimia 42.31 ya kura katika uchaguzi wa Jumamosi.Raia wa Sri Lanka wapiga kura ya kumchagua rais
Mwanasiasa huyo amembwaga kiongozi wa upinzani Sajith Premadasa aliyeshika nafasi ya pili na Wickremesinghe akimaliza katika nafasi ya tatu kwa mbali. Dissanayake anatarajiwa kuapishwa kesho Jumatatu. Kinyang'anyiro hicho kililazimika kuingia katika duru ya pili ya kuhesabu kurakati ya Dissanayake na Premadasa baada ya duru ya kwanza kumalizika bila mshindi kwa asilimia 50.