Dola Bilioni 2.2 zaahidiwa mkutano wa nishati safi Afrika
15 Mei 2024Shirika la Umoja wa Mataifa linashughulikia nishati IEA limetangaza kwamba serikali na makampuni duniani yameahidi kuwekeza kiasi dola bilioni 2.2 kusaidia upatikanaji wa nishati safi na salama ya kupikia barani Afrika.
Tangazo hilo limetolewa baada ya kukamilika kwa mkutano uliowaleta pamoja viongozi wa mataifa 60, wakuu wa taasisi za maendeleo na makampuni makubwa ya kibiashara kujadili njia za kumaliza tatizo la ukosefu wa nishati rafiki ya kupikia barani Afrika.
Mwishoni mwa mkutano huo uliofanyika mjini Paris, mkuu wa shirika la IEA Fatih Birol amesema mkusanyiko huo umetoa ahadi ya uhakika ya kushughulikia suala ambalo limepuuzwa kwa muda mrefu.
Zaidi ya watu bilioni mbili duniani wengine kutoka Afrika bado wanatumia majiko ya mkaa au kuni kupikia, njia ambazo zimekuwa na athari za kiafya na mazingira.
Fedha zilozoahidiwa kwenye mkutano wa Paris zinalenga kuzisaidia jamii kuanza kutumia njia rafiki kama gesi asilia au majiko ya umeme.