1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Dola bilioni 4 zakusanywa kuisaidia Syria

Sylvia Mwehozi
26 Aprili 2018

Wafadhili wa kimataifa wamekusanya Dola bilioni 4.4 kama msaada wa dharura kwa Syria na majirani zake, lakini kiasi hicho kimeshindwa kufikia lengo la Umoja wa Mataifa mwaka 2018 baada ya Marekani kutotowa ahadi yake. 

https://p.dw.com/p/2wi5o
Syrien-Geberkonferenz in Brüssel
Picha: Getty Images/AFP/E. Dunand

Mashirika ya kimsaada pia yametoa wito wa amani kabla ya jeshi la Syria na washirika zake Urusi na Iran kulishambulia eneo linalodhibitiwa na waasi kwenye mji wa Idlib, yakionya kwamba raia wapo katika mateso ya kiwango kikubwa kuliko ilivyokuwa wakati wa mzingiro wa Aleppo mwaka jana.

Naibu katibu mkuu wa masuala ya misaada ya kibinadamu wa Umoja wa Mataifa, Ursula Mueller, jana Jumatano amewaeleza wajumbe wa baraza la usalama la umoja huo juu ya mgogoro unaoendelea nchini Syria.

"Tunapaswa kuona hatua imara zikichukuliwa kuhakikisha kwamba pande zote zinaheshimu sheria za vita. Wananchi  lazima wapewe ulinzi na uagalizi wa mara kwa mara ili kuwaokoa na miundombinu wanayotegemea. mashambulizi ya hospitali hasa ni lazima yakome", alisema Ursula Mueller.

Syrien-Geberkonferenz in Brüssel Federica Mogherini
Mkuu wa sera za nje wa Umoja wa Ulaya Federica MogheriniPicha: Getty Images/AFP/E. Dunand

Uingereza na Ujerumani zilitoa fedha mpya kwa ajili ya wakimbizi katika mkutano huo, uliowaleta pamoja karibu serikali 85 na makundi ya misaada. Lakini ahadi hizo zilikuwa chini kwa dola bilioni 6 zilizokusanywa mwaka 2017 wakati rais Donald Trump akipunguza misaada ya kigeni. Mark Lowcock aliye mratibu wa misaada ya dharura ya Umoja wa Mataifa anasema,

"Wafadhili kadhaa muhimu bado hawajathibitisha ufadhili wao mwaka 2018 kwasababu ya hali ya majadiliano ya bajeti ya ndani, na hiyo inajumuisha Marekani iliyokuwa inatoa zaidi ya dola bilioni moja kwa mwaka kwenye misaada ya kibinadamu Syria na ukanda huo miaka ya karibuni."

Wakati Umoja wa Mataifa ukisema kwamba fedha zaidi zinaweza kujitokeza, serikali ya Marekani inaangalia upya sera yake ya Syria, ikiwemo misaada ya kiutu na Trump amehoji juu ya thamani ya misaada kama hiyo wakati akiendeleza ajenda yake ya "Marekani kwanza".

Syrien-Geberkonferenz in Brüssel Bundesaußenminister Maas
Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Heiko Maasbkatika mkutano wa kuisaidia SyriaPicha: Getty Images/AFP/E. Dunand

Umoja wa Ulaya sambamba na Marekani ambao ndio wafadhili wakubwa wa misaada  duniani  pia wanajitahidi kukubaliana na serikali zake wanachama kiasi cha yuro bilioni 3 katika mfuko wa kuwasadia wakimbizi nchini Uturuki.

Na wachunguzi wa silaha za kemikali wamekusanya sampuli siku ya Jumatano kutoka eneo jipya kwenye mji wa Syria wa  Douma, ikiwa ni ziara yao ya pili kwenye eneo lililoshambuliwa kwa gesi ya sumu karibu wiki tatu zilizopita.

Shirika  la kuzuia matumizi ya silaha za kemikali OPCW limesema sampuli zilizochukuliwa na timu ya wachunguzi mjini Douma zitatumwa katika maabara za shirika hilo kwa uchambuzi.

Mawaziri wa mambo ya kigeni wa Urusi, Iran na Uturuki wanatarajiwa kukutana siku ya jumamosi mjini Moscow kwa mazungumzo kuhusu hali  ya mambo nchini  Syria.

Mwandishi: Sylvia Mwehozi/ap/reuters

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman