Dortmund na Bremen zalenga kujikwamua
19 Desemba 2014Mbili kati ya timu zenye mafanikio makubwa katika Bundesliga, Werder Bremen na Borussia Dortmund, zinajikuta katika hali ya mapambano ya kujiondoa katika eneo la kushushwa daraja wakati zitakapokutan ana kwa ana hii leo.
Bremen na Dortmund zinayumba katika nafasi ya mkia wakati Bremen wakiwa na points 14 nao BVB wakiwa wa tatu kutoka nyuma na points 15. Timu zote mbili zimekuwa hasimu wa Bayern kwa miongo miwili iliyopita, lakini Bremen wako katika mchakato wa kujiimarisha baada ya miaka 14 chini ya kocha Thomas Schaaf na miaka ya mafanikio ya mwishoni mwa 80 na nusu ya kwanza ya miaka ya 90 chini ya Otto Rehhagel.
Ushindi wa mwisho wa ubingwa wa Bundesliga wa Bremen mwaka wa 2004 ulikatiza mfululizo wa mataji ya Bayern ya 2003,2005 na 2006 wakati ushindi wa Dortmund wa 2002 ulikuja katikati ya ushindi mara nne wa Bayern kutoka 1999 na 20013. Hivi karibuni, mataji ya BVB ya 2011 na 2012 yalitia kikomo mafanikio ya Bayern ambayo yalirejeshwa tena katika misimu miwili iliyopita na yanatarajiwa kuendelea kwa kupata taji la tatu mfululizo.
Mahasimu wa Bremen katika upande wa kaskazini SV Hamburg, ambao wana points 16 wana mchuano mgumu ugenini dhidi ya nambari tano Schalke, wakati VfB Stuttgart ambao wana points sawa baada ya kuwazaba Hamburg goli moja kwa sifuri katikati ya wiki, watakutana na Paderborn ambao wana points 18. Freiburg, walio na points sawa na Bremen wanakabiliana na Hanover kesho Jumapili. Mechi nyingine ya kesho Jumapili ni kati ya Hertha Berlin watakaowatembelea Hoffenheim.
Wolfsburg ambao wako katika nafasi ya pili nyuma ya Bayern watacheza ugenini leo dhidi ya Cologne. Nambari tatu Borussia Moenchengladbach pia leo watakuwa wenyeji wa Augsburg, wakati Bayer Leverkusen, walio na points sawa na Gladbach, wakicheza nyumbani dhidi ya Eintracht Frankfurt.
Mwandishi: Bruce Amani
Mhariri: Mohammed Abdulrahman