1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Dortmund, Schalke zaanza msimu kwa kichapo

26 Agosti 2014

Goli la haraka kuliko yote yaliyowahi kufungwa katika sekunde za mwanzo za mchezo yamezamisha makamu Borussia Dortmund katika mchezo wao wa kwanza katika msimu mpya Bundesliga

https://p.dw.com/p/1D0v6
Borussia Dortmund vs Bayer Leverkusen
Picha: Christof Koepsel/Bongarts/Getty Images

Kikosi cha kocha Jurgen Klopp kilikubali kipigo cha mabo 2-0 dhidi ya Bayer Leverkusen. Mshambuliaji wa Leverkusen Karim Bellarabi alipachika bao sekunde tisa baada ya mchezo kuanza na kuiyumbisha kabisa Dortmund ambao hawakuweza tena kurejea katika mchezo wao, na katika dakika 5 za majeruhi mwishoni mwa mchezo huo Kiessling alipachika bao la pili kwa Leverkusena na kupiga msumari wa mwisho katika jeneza la Dortmund jioni hiyo.

Mfungaji wa bao hilo Karim Bellarabi alisema. "Nimesikia hivi punde tu kwamba hiyo ni rekodi mpya. Ninafarijika sana kusikia hivyo, lakini cha muhimu ni kwamba tumeshinda mchezo huu. Ndio sababu nina furaha kubwa."

Schalke 04 hoi

Baada ya kutolewa katika duru ya kwanza katika kombe la shirikisho DFB Pokal na timu ya daraja la pili ya Dynamo Dresden , Schalke 04 haikuwa na jibu katika mchezo wa kwanza wa Bundesliga siku ya Jumamosi wakati walipobamizwa mabao 2-1 na Hannover 96. Nahodha wa Schalke 04 Benedict Höwedes alijiliwaza kwa kusema.

Hannover 96 - FC Schalke 04
Eric Maxim Choupo-Moting ( Schalke ), kushoto akimenyana na Leonardo Bittencourt ( Hannover )Picha: picture-alliance/dpa

"Msimu ndio kwanza unaanza. Tumeuanza msimu huu tofauti kabisa na tulivyopanga. Hii itasababisha maneno mengi kusemwa lakini tuliwahi pia kupata matatizo makubwa na kufanikiwa kubadilisha mambo, na kuweza kujionesha kuwa sisi ni timu imara. Na tutafanya hivyo mara hii pia. Kwa hiyo kwangu mimi hilo halisumbui kichwa."

Bayern yaponea chupu chupu

Mabingwa watetezi Bayern Munich wameponea chupu chupu kupoteza point nyumbani wakati walipokumbana na VFL Wolfsburg katika mchezo wa ufunguzi wa ligi hii ya mabingwa wa kombe la dunia katika msimu huu wa 52, baada ya kupata ushindi mwembamba wa mabao 2-1 na mshambuliaji wa Wolfsburg Junior Malanda kukosa bao ambalo huenda likawa gumzo kubwa msimu mzima akiwa yeye na msitari wa mwisho wa goli la Bayern. Ilikuwa katika dakika za majeruhi katika mchezo huo na mabao yakisomeka 2-1 kwa Bayern.

Bundesliga Bayern München - VFL Wolfsburg Götze
Mario Goetze wa Bayern akipambana na mchezaji wa Zamani wa Bayern Luiz Gustavo wa WolfsburgPicha: Getty Images

Borussia Moechengladbach imenusurika nayo kupoteza mchezo jana Jumapili wakati ilipopata bao la kusawazisha katika dakika ya 90 ya mchezo huo bao lililofungwa na mchezaji chipukizi wa timu ya taifa Christoph Kramer ambaye alionesha furaha yake kwa kusema.

"Kwa kweli ni jambo zuri sana, kwamba nimeweza kufunga bao tena. Kwa hiyo katika michezo mitatu ya mashindano nimeweza kufunga mabao kwa timu yangu ya Moenchengladbach. Nataka kujaribu kadri ya uwezo wangu kutumbukiza mpira wavuni vizuri. Kwamba mpira unakwenda vizuri wavuni , ni kwa kiasi fulani bahati tu. Lakini pamoja na hayo nimefurahi sana."

Mchezo huo kati ya Borussia Moenchengladbach na VFL Stuttgart ulimalizika kwa sare ya bao 1-1. Katika mchezo wa kwanza hapo jana Jumapili (24.08.2014)timu iliyopanda daraja msimu huu SC Paderborn ilitoka sare ya mabo 2-2 na Mainz 05.

Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe / rtre / ape /dpae / zr /
Mhariri: Josephat Charo