Dortmund yaivuka Hoffenheim katika nafasi ya tatu
8 Mei 2017Katika Bundesliga katika mchezo wa 32 wiki hii kulikuwa na msuguano mkubwa kati ya Borussia Dortmund na TSG Hoffenheim kuwania nafasi ya tatu inayohakikisha timu itakayonyakua nafasi hiyo kushiriki katika awamu ya makundi katika Champions League pamoja na tuzo ya euro milioni 30. Uhakika wa kupata tuzo hiyo ndio uliufanya mchezo huo kuwa muhimu sana, ikitiliwa maana kwamba timu itakayoteleza kwenda nafasi ya nne itabidi kuingia katika michezo ya mchujo kabla ya kuingia katika awamu ya makundi ya Champions League.
Na hii Hoffenheim ilitaka kuepuka kwa kuwa ni timu isiyokuwa na uzoefu katika jukwaa hili la kimataifa , na huenda ikakumbana na baadhi ya vigogo katika bara la Ulaya kama kutoka Itali, Uingereza na Uhispania katika kinyang'anyiro hicho cha mchujo.
Borussia Dortmund ikicheza nyumbani iliibuka kidedea kwa ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Hoffenheim , lakini kwa kweli kulitokea makosa mengi yaliyofanywa na mwamuzi wa mchezo huo Dr. Felix Brych ambaye ni refa bora kabisa nchini Ujerumani na hata Ulaya kwa jumla. Alifanya makosa mara mbili ambapo aliruhusu bao la kwanza la Borussia Dortmund alilofunga Marco Reus akiwa katika nafasi kabisa ya kuotea. Pili aliwapa Dortmund mkwaju wa penalti wakati kabla ya hapo Marco Reus alionekana kuutuliza mpira kwa sehemu ya mkono wake karibu na bega. Mkwaju huo wa penalti uliopigwa na Pierre Emerick Aubameyang hata hivyo uliishia nje ya wavu. Huyu hapa Marco Reus akizungumzia matukio hayo katika mchezo huo.
"Sidhani kama refa alitupendelea, kinyume chake kabisa. Lakini ni bila shaka , ikiwa niko mita moja katika nafasi ya kuotea, ni lazima aamue haki, kwa hiyo ulikuwa uamuzi wa makosa. Naamini , katika msimu huu tumepata pia kuadhibiwa kimakosa, ambapo hatukuchukulia kwamba mwamuzi ndio aliyesababisha hilo. Kwa hiyo nadhani kila kitu kiko sawa."
Hata hivyo kocha wa TSG Hoffenheim Julian Nagelsmann hakuna cha kumtuliza kutokana na makosa yaliyotokea katika mchezo huo.
"Mshika kibendera alithibitisha kwamba goli hio llikuwa ni la kuotea. Lakini amenithibitishia kwamba , mwamuzi ndio aliyeshikilia kwamba ni goli na si yeye. Pengine hakuwa na uwezo wa kumshawishi mwamuzi. Ninapoangalia jinsi mchezo ulivyokuwa kati ya kikosi changu na Dortmund , mchezo wetu ulikuwa bora zaidi, na ndio sababu ningetarajia zaidi ushindi."
Bado kuna michezo miwili kabla ya kumalizika kwa msimu huu wa Bundesliga , na timu hizo zinakumbana katika michezo hiyo miwili na timu mbili Werder Bremen na Augsburg. Borussia Dortmund inasafiri kwenda kupambana na Augsburg siku ya Jumamosi ijayo, wakati TSG Hoffenheim nayo inasafiri kwenda kupambana na Werder Bremen nyumbani.
Mbali ya pambano hilo lililochukua hisia za mashabiki wa kandanda nchini Ujerumani , lakini pia klabu ya kandanda ya SV Damstadt 98 kwa shingo upande ilibidi kutoa mkono wa kwaheri kwa Bundesliga , baada ya kupokea kipigo cha bao 1-0 kutoka kwa mabingwa wateule Bayern Munich licha ya wao kukosa penealti katika dakika ya 86 ambapo mchezaji wa zamani wa Bayern Hamit Altintop alishindwa kuuweka mpira wavuni ambapo ulipanguliwa na mlinda mlango Tom Starke. Baada ya kudumu kwa miaka miwili katika Bundesliga klabu hiyo inayotoka katika jimbo la Hessen kulazimika kushuka daraja.
Hiyo ni timu ya kwanza kushuka daraja msimu huu, lakini mapambano ya kuwania kubakia katika daraja hilo yanaendelea.
Wolfsburg imepiga hatua kuelekea kubakia katika daraja la kwanza kwa kuikandika Eintracht Frankfurt kwa mabao 2-0 , na kuziacha FSV Mainz iliyoko katika nafasi ya 15 na SV Hamburg iliyoko katika nafasi ya 16 kubakia na pointi 34 zikiwania nafasi ya 16 ambayo inahusika na mchujo wa kubakia katika daraja la kwanza. Timu hizo zilitoshana nguvu jana Jumapili na kumaliza mchezo wao bila kufungana.
Kwa upande mwingine mbio za kuwania kucheza katika ligi ya Ulaya , Europa League zinaendelea , wakati SC Freiburg imekoleza moto jana baada ya kuishinda Schalke 04 kwa mabao 2-0 , hali inayoikatisha tamaa Schalke kucheza Ulaya msimu ujao. Mchezaji wa kati wa Schalke 04 Leon Goretzka alikuwa na haya ya kusema.
"Baada ya kufungwa bao la pili katika kipindi cha kwanza Freiburg ilijiweka katika nafasi nzuri sana. walitufanya tushindwe kabisa kucheza mchezo wetu, licha ya kuwa walicheza nyumbani na hii kwa kweli imetuathiri sana msimu huu."
Hertha BSC Berlin ilipokea kipigo cha mabao 4-1 siku ya Jumamosi na matumaini yao ya kucheza kombe la ligi ya Ulaya pia yanalegalega , kama ilivyo kwa FC Kolon ambayo licha ya kuishinda Werder Bremen kwa mabao 4-3 siku ya Ijumaa sasa imefikisha pointi moja nyuma ya Hertha Berlin kuweza kufikia nafasi hiyo ya kucheza kombe la ligi ya Ulaya.
Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe / rtre / dpae
Mhariri: Josephat Charo