Dortmund yapanda hadi nafasi ya pili
29 Novemba 2012Bayer Leverkusen imepata ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya TSG Hoffenheim na kujiimarisha katika nafasi ya tano ya msimamo wa ligi. Kwa ushindi wa jana wa kikosi cha kocha Sascha Lewandowski unakuwa ushindi wa saba katika msimu huu.
FC Augsburg na Borussia Moenchengladbach hazikuonyesha wa kusisimua sana jana na waliridhika na sare ya bao 1-1.
Ushindi mnono ulikwenda kwa SC Freiburg, ambapo iliizaba VFB Stuttgart kwa mabao 3-0 na Freiburg ikachupa hadi nafasi ya sita katika msimamo wa ligi.
Dortmund yakwea juu
Borussia Dortmund , ambao ndio mabingwa watetezi wa ligi hiyo wametoka nafasi ya nne na kuchipa hadi nafasi ya pili, ikiwa sasa inaiwinda Bayern Munich, ambayo siku ya Jumamosi ilifanya mauaji makubwa dhidi ya Hannover 96 kwa kuichapa mabao 5-0 nyumbani.
Dortmund ilihitaji kufanyakazi ya ziada kupata ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya majirani zao wa Mainz 05.
Pambano lililokuwa likisubiriwa kwa hamu hata hivyo ni kati ya VFL Wolfsburg ambayo ikiwa na meneja mpya Klaus Allofs ilikuwa inapambana na Werder Bremen ambayo ni wiki iliyopita tu meneja huyo alikuwa akiitumikia. Mpambano huo uliongezwa hamasa na kuhama kwa Klaus Allofs kutoka Werder Bremen na kwenda VFL Wolfsburg. Hata hivyo pambano hilo lilimalizika kwa sare ya bao 1-1.
Real yateleza
Huko nchini Hispania, mabingwa watetezi Real Madrid waliteleza pale walipokubali kipigo cha bao 1-0 dhidi ya Real Betis, ikiwa ni kipigo cha tatu katika kampeni ya msimu huu kwa kikosi cha kocha Jose Mourinho.
Viongozi wa ligi hiyo Barcelona pamoja na timu iliyo katika nafasi ya pili Atletico Madrid wamefanikiwa kuweka kasi yao ya kusonga mbele jana, wakati Barca ilipoibamiza Levante kwa mabao 4-0 na Altelico ikainyuka Sevilla kwa kiwango kama hicho cha mabao 4-0.
Katika Premier League Manchester United ilifanikiwa kurejea kileleni mwa msimamo wa ligi baada ya ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Queens Park Rangers, wakati mabingwa Manchester City wakiridhika na sare ya bila kufungana na Chelsea . Kocha Rafa Benitez alikuwa akisimamia mchezo wake wa kwanza baada ya kurejea katika Premier League. Mapokezi ya Benitez kwa mashabiki wa Chelsea hayakuwa mazuri, wengine wakipaaza sauti kuwa hatakiwi katika klabu hiyo na wengine wakitabiri kuanguka kwake kwa haraka. Mashabiki walikuwa katika mchezo huo wakimwagia sifa na kuimba jina la kocha wa zamani aliyetimuliwa Roberto Di Matteo.
Lakini Benitez anadai kuwa hana wasi wasi kwa kuwa ushindi utawafanya mashabiki hao kusafiri nae katika ngalawa moja.
Huko Italia viongozi wa ligi ya Italia, Serie A ambao pia ndio mabingwa watetezi Juventus Turin wameangukia pua jana kwa kipigo cha bao 1-0 dhidi ya AC Milan kwa bao la penalti la Robinho.
Juve inaongoza kwa kuwa na points 32 kutoka michezo 14 huku Inter Milan ikiwa nyuma kwa points nne kabla ya pambano lao hii leo Jumatatu dhidi ya Parma. Fiorentina iliyo katika nafasi ya tatu ilitosheka na sare ya mabao 2-2 dhidi ya Torino jana Jumapili.
Paris St Germain inaongoza ligi ya Ufaransa ikifuatiwa na Olympique Marseille kwa tofauti ya magoli, na timu hiyo ina miadi na Olympique Lyon siku ya Jumatano.
Bundesliga yarejea tena uwanjani
Ligi ya Ujerumani Bundesliga inarejea uwanjani kesho jioni ambapo timu zitaingia uwanjani katika mchezo wa 14 wa ligi hiyo. Mabingwa watetezi Borussia Dortmund itakuwa na kibarua na Fortuna Düsseldorf, Frankfurt itakuwa nyumbani ikiwakaribisha Mainz 05, Hannover iliyojeruhiwa siku ya Jumamosi itatafuta njia ya kulipiza kisasi dhidi ya Greuther Fürth na Hamburg SV ina miadi na Schalke 04.
Jumatano itakuwa zamu ya Stuttgart ikikwaana na FC Augsburg, Werder Bremen ikitiana kifuani na Bayer Leverkusen , Borussia Moenchengladbach inakwaana na VFL Wolfsburg , Freiburg inawakaribisha viongozi wa ligi hiyo Bayern Munich nyumbani, wakati Nurnberg itaonyeshana kazi na Hoffenheim.
Na mashindano ya kuwania ubingwa wa mataifa ya Afrika mashariki na kati yameanza rasmi huko mjini Kampala Uganda, ambapo timu za mataifa 12 ya Afrika mashariki na kati zinapambana. Wenyeji wa mashindano hayo Uganda imeanza vizuri kwa ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Kenya, na Kilimanjaro Stars ya Tanzania imeibwaga Sudan kwa mabao 2-0 jana Jumapili(25.11.2012), wakati Burundi ilipitisha mipira mara tano katika nyavu za Somalia . Somalia iliambulia bao moja. Katika pambano kati ya Zanzibar na Eritrea, matokeo ni sare ya bila kufungana. Mchezo wa pili ni kati ya Rwanda na Malawi.
Mascot
Kila mashindano ya fainali za kombe la dunia kunakuwa na kinyago cha kuleta bahati, maarufu kama mascot. Katika fainali za kombe la dunia mwaka 2014 nchini Brazil kinyago hicho kimepewa jina la Fuleco, zoezi lililofanywa kwa ushirikiano wa mashabiki wa soka nchini humo , limesema shirikisho la kandanda duniani FIFA leo.
FIFA imesema kuwa asilimia 48 ya Wabrazil waliohusika katika kura hiyo wamechagua jina la Fuleco kuwa jina hilo, wakati Zuzeco limepata asilimia 31 na Amijubi limepata asilimia 21.
Fuleco ni mchanganyiko wa maneneo Futebol, yaani kandanda na ecologia yaani mazingira na FIFA imesema uchaguzi huo unaonyesha kuwa Wabrazil wanajali mazingira kama wanavyojali kuhusu soka. Kinyago hicho kinatokana na umbo la mnyama mwenye asili ya Brazil anayejulikana kama Armadilo , na kilichotakiwa ni armadilo kupata jina.
Wakati huo huo Wajerumani wamesherehekea ushindi wa dereva bora katika mbio maarufu za magari za Formula 1, ambapo Sebastian Vettel alipata ushindi wake wa tatu katika historia ya mbio hizo. Dereva huyo wa kundi la Red Bull alimaliza akiwa wa sita katika mbio hizo zilizofanyika nchini Brazil.
Lakini kundi la magari ya Ferrari limesisitiza kuwa Vernando Alonso , ambaye ameshika nafasi ya pili , alipaswa kuwa mtu anayesherehekea ushindi wa tatu, wakielekeza kidole kwa mbio zenye utata zilizofanyika nchini Ubelgiji na Japan katika kuelezea hisia zao.
Kwa taarifa hiyo ya mbio za magari ndio sina budi kusema tumefikia mwisho wa kuwaletea habari hizi za michezo kwa leo. Jina langu ni Sekione Kitojo, hadi mara nyingine kwaherini.
Mwandishi : Sekione Kitojo / rtre / afpe / dpae
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman